
Dar es Salaam. Wanawake wanaofanya kazi katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wametakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea rushwa na watendaji wazembe ili kuwapatia wananchi huduma ya umeme iliyo bora.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Machi 4,2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko, katika kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme kwa wanawake wa shirika hilo.
Kongamano hilo limewakutanisha wanawake wa shirika hilo kutoka maeneo yote nchini ikiwa ni shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake ambayo huadhinishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka.
Akizungumza na wanawake hao ambapo alikuwa mgeni rasmi, Dk Biteko amesema wananchi wanatamani shirika hilo liwahudumie, hivyo wanapoona mtu anamuomba mteja rushwa ili aunganishiwe umeme wawe wa kwanza kumkemea.
“Nilipata simu kuna mtumishi analalamikiwa na mteja alipotaka kwenda kumuunganishia umeme, alimwambia ampe hela ya kuweka mafuta gari. Msikubali watu hawa wachache wawaharibie jina na sifa ya shirika hili,” amesema Dk Biteko.
Amesema kwa kufanya hivyo pia watawasaidia wanawake wenzao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia nishati chafu kupikia waanze kupikia nishati hiyo safi ya umeme ambayo wengi wao wanadhani ni kwa ajili ya kuwashia taa tu.
Katika hatua nyingine Dk Biteko amesema amekoshwa na namna ambavyo Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gassima Nyamo Hanga, alivyofanyia kazi maagizo yake ya kuwepo kwa wanawake katika safu ya juu ya uongozi.
Ameeleza kuwa mara ya kwanza alipoteuliwa na kwenda kutembelea shirika hilo, viongozi wote wa juu waliokuwa naye meza kuu walikuwa wanaume, na mwanamke aliyemuona ni yule aliyekuwa akitoa huduma ya maji ya kunywa jambo ambalo halikumpendeza na kutaka hilo lifanyiwe kazi.
“Nashukuru leo naambiwa katika safu ya wakurugenzi 12, wanne ni wanawake japo kazi bado tunayo hapa kuhakikisha tunakuwa na usawa katika nafasi hizi kwa kuwa naamini wanawake wenye uwezo wapo,” amesema Dk Biteko.
Amesema mmoja wa mwanamke wa mfano ni naibu wake Judith Kapinga ambaye ameeleza wakati anateuliwa kuwa msaidizi wake alikuwa na mtoto mchanga.
“Pamoja na mama huyu kuwa na mtoto mchanga haikuwa kikwazo kwake kufanya kazi nilizokuwa namuagiza, kwani kila niliyomwambia aliniambia ndio mheshimiwa hiyo nitaifanya na aliifanya kweli,”amesema Dk Biteko.
Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, amesema ni ubunifu mzuri waliokuja nao viongozi kwa kuwakutanisha wanawake wote wa shirika na kujadili mambo yao, huku akiwataka wawe vinara wa kutumia nishati hiyo ya umeme katika kupikia.
Katika kulitekeleza hilo, amemtaka mkurugenzi kuangalia namna ya kuwapatia fedha wanunue majiko ya umeme ili wanapoitoa elimu hiyo kwa wengine, wao wawe mfano badala na wao wakitoka hapo wanaenda kutafuta wapi mkaa ulipo.
Waziri huyo amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuunga Rais Samia Suluhu Hassan ajenda yake ya matumizi ya nishati safi, ambayo amekuwa kinara sio ndani ya nchi bali hata nje ya mipaka.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Judithi Kapinga amesema kwa kuwa ajenda hiyo ya matumizi ya nishati safi ni ya Rais Samia, wanawake nao hawana budi kumuunga mkono.
Katika ajenda hiyo, Serikali inataka ifikapo mwaka 2030 asilimia 75 wawe wamefikiwa na nishati safi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, amesema wamefarijika kuona teknolojia ya majiko ya umeme ya kisasa yasiyotumia umeme mwingi katika maonyesho yaliyokuwepo kwenye kongamano hilo.
Twange amesema kilichobaki ni wao kama viongozi sasa kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu teknolojia hiyo, ukizingatia gharama ya matumizi yake ni rahisi kuliko ya kununua mkaa.
Nyamo Hanga, amesema watu wengi huko nyuma waliamini kwamba kupikia umeme ni gharama kubwa.
“Pia, vijiji vingi sasa vimefikiwa na umeme na shughuli nyingi za kiuchumi zinafanywa kwa nishati hiyo, hivyo naomba niwaondoe woga wananchi kuhusu kutumia umeme kupikia,”amesema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Zuhura Bundala, amepongeza waliokuja na wazo hilo la kongamano na kuwahusisha wanawake, akisema anaamini watafikisha elimu waliyoipata kwa ndugu zao.
Zuhura ameahidi kuwa bodi itaendelea kusimamia miradi yote ya nishati ya umeme kwa nguvu kubwa, huku akiwataka wananchi kutoogopa kutumia nishati hiyo kwa kuwa ni nyingi nchini na wanachopaswa ni kuitumia kwa wingi pia.
“Kwa sasa nchi ina umeme mwingi na ndoto za kuwa na umeme mwingi kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere inaenda kutimia, hivyo ni vizuri pia kuongeza matumizi.”
Awali, mratibu wa kongamano hilo, Irene Gowelle, amesema lengo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme.
“Katika uhamasishaji huo tumeona tusiende nje kwanza bali tuanzie ndani kwa wanawake wa Tanesco kuona namna gani matumizi ya nishati safi ni mkombozi kwa mwanamke,”amesema Irene ambaye pia ndio Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Tanesco.