
Watafiti wamebaini wanaume huchoma zaidi mafuta mwilini wakati wa tendo la ndoa kuliko wanawake.
Ni kweli wakati wa tendo hilo, wote hupata raha, lakini ni raha ya kuvuja jasho huku wanaume wakitajwa kumenyeka zaidi hasa pale wanapohitaaji kuwaridhisha wake zao.
Utafiti huo umeonyesha wanaume huchoma kalori 101 wakati wa mapenzi huku wanawake wakichoma kalori 69 pekee.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya na tiba kwa wanawake kutoka Marekani, Leah Millheiser, wanaume ndio mara nyingi hujizatiti sana kitandani wakati wa kitendo cha kujamiiana.
Kujizatiti kwao kunaweza kufasiriwa au kulinganishwa na kufanya mazoezi ndipo hapo anaposema wao hufikia hatua ya kuchoma mafuta zaidi mwilini.
“Kuna tofauti kati ya tendo la ndoa ambalo huchukua dakika tano lakini ni la kasi ya juu kuliko lile ambalo hudumu kwa saa kadhaa. Kila mtu huwa na hali tofauti kuhusiana na hili,” alisema mtaalamu mwingine Emily Morse kwenye mahojiano yaliyonakiliwa na jarida la The Newyork Post.
Hata hivyo, tendo la ndoa linaweza kufasiriwa kama mazoezi au kazi kutegemea mambo kadhaa yakiwamo mtindo, muda na mahali ambapo mume na mke au wapenzi wanajaamiana.
“Iwapo unataka kudumu sana kitandani na kuchoma mafuta kupitia kutokwa jasho jingi, basi ni vyema wapenzi wajaribu mitindo mipya ya kufanya tendo,” anasema mtaalamu wa masuala ya mapenzi, Jaimee Bell.
Hata hivyo, mafuta yanayochomwa mwilini wakati wa ngono ni madogo ikilinganishwa na yale ambayo yangemalizwa mwilini wakati wa mazoezi ya kawaida.
“Mbali na kuongeza kasi ya kupumua, mapigo ya moyo na shinikizo la damu wakati wa kushiriki tendo, inaonekana kufanya mapenzi hakuwezi kuchukuliwa kama sehemu ya mazoezi. Hii ni kwa sababu manufaa yake ni madogo kilinganishwa na kukimbia, kuendesha baiskeli na kuinua vitu vizito,” anasema mwanasayansi, Dkt Jason Karp.