Wanasaikolojia watoe huduma ya afya ya akili ngazi zote

Serikali imetoa mwelekeo mpya wa kuanza mchakato wa kutunga sheria ya uanzishwaji wa Baraza la Afya ya Akili ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kikamilifu kwa mujibu wa Sheria ya Kusimamia Afya ya Akili nchini ya mwaka 2008.

Kauli ya Serikali kuhusu kuanza mchakato huo ni hatua nzuri kuelekea kukabiliana na tatizo la afya ya akili ambalo limeonekana kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Tunasema limeongezeka kutokana na kukithiri kwa matukio ya kikatili katika jamii, ambayo yanatajwa yanatokana na tatizo la afya ya akili.

Suala la ukatili wa kudhuriana kwa kupigana na kuuana miongoni mwa wanajamii, watu kuwa na hasira, wasiwasi, kutukana mitandaoni, kutojiamini ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kushamiri, ikitajwa kuwa ni chanzo cha matatizo ya akili.
Dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Akili ifikapo Oktoba 10 kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ‘Ni wakati wa kuipa kipaumbele afya ya akili mahali pa kazi’.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha takribani watu bilioni 1 duniani wanakabiliwa na tatizo la afya ya akili na Tanzania ikiwemo.

Mtaalamu wa afya ya akili na mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Semeni Lukaga amewahi kuhojiwa na gazeti hili na kueleza kwamba watu wengi wanaathirika kupitia mitandao ya kijamii kwa kuangalia maisha ya watu wengine namna wanavyoweka picha mitandaoni kuhusu maisha yao na namna wanavyofanya starehe.

Hali hiyo inawafanya baadhi kuanza kuathirika bila kujijua, na kuanza kuumia akilini na kujiona wana maisha duni, hivyo taratibu wanaanza kujiona wana maisha duni.

Hoja yetu ni kuonyesha vyanzo vya tatizo na kuitaka Serikali kushughulikia maeneo mengine yote ambayo yanasababisha watu kuingia kwenye matatizo ya afya ya akili.

Suala la ajira kwa wananchi, haki katika taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi, usawa wa kijinsia, kushughulikia umasikini uliokithiri kwa wananchi, hayo ni maeneo muhimu yanayopaswa kushughulikiwa.

Itakumbukwa kwamba suala la afya ya akili liligusiwa pia na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ripoti yake ya mwaka 2022/2023, alipofanya ukaguzi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

Miongoni mwa mapendekezo yake yalikuwa ni; kuboreshwa huduma za afya ya akili, kutoa elimu ya afya ya akili, kuwepo sera, kuboreshwa sheria, huduma zipatikane nchini kote, huduma za kisaikolojia ziingizwe katika bajeti na mipango ngazi mbalimbali.

Ni rai yetu, juhudi ziongezwe katika kutoa huduma za matibabu ya afya ya akili na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa gharama nafuu katika hospitali za Serikali ambazo zinatoa huduma kwa watu wenye tatizo la afya ya akili.

Kupitia baraza hilo ambalo Serikali imeanza mchakato wa kuliunda, uwekwe umuhimu mkubwa kuwepo wanasaikolojia kuanzia ngazi za serikali za mitaa, kata hadi wilayani.

Vilevile Serikali itoe tamko kuhusu ulazima wa upatikanaji wa huduma za wanasaikolojia katika maeneo ya kazi, shuleni, vyuo vya kati na vyuo vikuu hata kwenye maeneo mengine ya huduma za kijamii.

Kwa kufanya hivyo, itasaidia kukomesha matukio ya kikatili yanayotokana na watu kuwa na hasira, chuki zinazotokana na tatizo la afya ya akili. Pia tutaweza kuwa na Taifa lenye watu wenye afya njema ya akili, wanaoweza kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji.