Dar es Salaam. Wafanyabiashara 651 kati ya 1520 wanaotakiwa kurejea soko Kuu la Kariakoo wameitwa kuonyeshwa na kugaiwa maeneo yao.
Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kuanza kazi tena kwa soko hilo ambalo liliunga Julai 2021.
Kutokana na janga hilo, Serikali ilitoa zaidi ya Sh29 bilioni kwa ajili ya ukarabati wake uliofanyika sanjari na ujenzi wa soko jingine jipya (soko dogo).
Katika kipindi chote cha ujenzi wafanyabiashara waliokuwa sokoni hapo walihamishiwa kwa muda katika masoko ya Karume, Machinga Complex na Kisutu.
Ikiwa imepita takribani miaka mitatu sasa uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo, umesema limeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 98 na lipo tayari kuanza shughuli zake mwezi huu wa Aprili.
Walivyowaita wafanyabiashara kuwapangia maeneo
Jana, Aprili 10, 2025 Shirika hilo lilituma orodha ya watu 651 katika masoko ambayo wafanyabiashara hao walihamishiwa na kuwataka wafika sokoni hapo leo Aprili 11, 2025 kwa ajili ya kuanza kugaiwa vizimba vyao.

Baadhi ya wafanyabiashara soko Kuu la Kariakoo wakiwa wamekusanyika nje ya soko hilo baada ya kugaiwa vizimba vyao leo Ijumaa Aprili 11, 2025.
Katika ufanyikaji wa shughuli hiyo wamewagawa wafanyabiashara hao katika makundi matatu A, B na C kila moja likiwa na watu zaidi ya 200
Kundi A lilipangwa kwenda kuonyeshwa maeneo saa 4:00 asubuhi, huku kundi B likitakiwa kwenda saa 7:00 mchana na kundi C lenyewe litagaiwa siku ya Jumanne Aprili 15,2025.
Hata hivyo Mwananchi Digital iliyokuwa imepiga kambi eneo hilo imeshuhudia kuibuka mvutano kati ya wafanyabiashara waliofika saa 4:00 asubuhi na uongozi wa soko baada ya kukataa watu wote wasiingie ndani.
Badala yake walioruhusiwa kuingia ni watu 20 wengi wao wakiwa viongozi.
Sababu ambazo wameambiwa na mmoja wa walinzi ni kwamba mkandarasi bado hajamaliza ujenzi hivyo isingekuwa rahisi kuwaruhusu kundi hilo la watu kuingia.
Sababu hii imethibitishwa pia na Msemaji wa Shirika hilo la Masoko, Revecatus Kasimba alipozungumza kwa njia ya simu.
“Ni kweli hatukuweza kuwaruhusu wafanyabiashara wote waingie kwa leo, kwa kuwa mkandarasi bado kuna maeneo alikuwa anaendelea na ujenzi hivyo kundi hilo lingeingia lote lingeweza kukanyaga na kuharibu maeneo hayo.
“Hivyo tulikubaliana na mkandarasi waingia wachache ambao wataenda kuwapa taarifa na wenzao na waliobaki tutaendelea nao wiki ijayo,” amesema Kasimba.
Hata hivyo msemaji huyo amesema lengo lao leo ilikuwa kuwakabidhi vizimba wafanyabiashara 500 na kuwapa mikataba ya upangishaji lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza wameshindwa na watafanya hivyo wiki ijayo.
Kwa mujibu wa Kasimba shughuli hiyo imepata baraka zote kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mkandarasi mshauri ambao ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo wanaopangiwa ni wale wa soko jipya (soko dogo).
Walicholalamikia wafanyabiashara
Wakitoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara waliofika sokoni hapo, wamesema walichokifanya shirika ni kuwapotezea muda.

Baadhi ya wafanyabiashara Soko Kuu la Kariakoo wakiwa wamekusanyika nje ya soko hilo baada ya kugaiwa vizimba vyao leo Ijumaa Aprili 11, 2025.
Mfanyabiashara aliyejitaja kwa jina moja la Amina, amesema baada ya kupata taarifa kwamba wanatakiwa alisafiri usiku saa nne akitokea lindi na alifika Dar es Salaam saa tisa usiku.
“Hapa ninavyokwambia nina usingizi, sijalala, lakini kwa kuwa ni jambo ambalo nilikuwa nalisubiri muda mrefu imebidi nijihimu nije, halafu mwisho wa siku ndio kama hivyo nimezuiliwa wanaambiwa wanaotakiwa kuingia ni watu 20.
“Kama walijua ndio hivyo kwa nini walituita watu wote, huu sio usumbufu wa kutupotezea muda tu bali na kutuingiza gharama zisizo za lazima,” amesema Amina.
Naye Habiba Kiyogoa, amesema waliambiwa leo waende na vitambulisho vya kura au vya uraia, na amefika hapo kabla ya saa nne.
Habiba amesema kama walitaka viongozi tu wangewaambia, kwani hata huko nyuma kwenye michakato mingine walikuwa wakiwahusisha wao na kisha kuwapelekea taarifa.
“Nimeacha shughuli zangu nimekuja kukaa hapa zaidi ya saa tatu, hii sio sawa,” amesema mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo amesema kiu yake ni soko lifunguliwe ndani ya mwezi huu kwa kuwa wengine waliamua kukaa nyumbani kutokana na maeneo waliyohamishiwa kutokuwa na biashara. Habiba alihamishiwa soko la Karume baada ya soko kuungua.
Ulinzi waimarishwa, walioingia wazungumza
Baadhi ya waliobahatika kuingia ndani ya soko hilo wamesema wamekabidhiwa vizimba.
Mfanyabiashara ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema katika kukabidhiwa huko kizimba unaulizwa jina lako na kitambulisho kisha unaambiwa namba ya kizimba chako ni fulani kisha unaenda kilipo.
Hata hivyo amesema hawajaridhika na utaratibu kwani wamepangiwa sakafu moja watu wanaofanya biashara tofauti.
Amesema hata walipohoji kwa uongozi wa soko kwa nini wamefanya hivyo waliambiwa huko baadaye ambaye atakuwa hajaridhika watabadilishana na mwingine.
“Haiwezekani mimi nauza mbogamboga ukaenda kunipanga na mtu anayeuza nafaka, lazima kuwe na utaratibu mzuri wa kutupanga nina imani hili litafanyiwa kazi kabla ya soko kuanza,” amesema mfanyabiashara huyo.
Katika hatua nyingine shughuli hiyo ilifanyika chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Mwananchi imeshuhudia ilishuhudia gari la polisi likiwa katika maeneo hayo ya soko na askari zaidi ya kumi baadhi wakiwa katika sare na wengine wakiwa wamevalia nguo za kiraia.
Polisi hao walisaidiana na walinzi wa eneo hilo katika kuwaingiza ndani ya geti wafanyabiashara walioteuliwa kuwawakilisha wenzao kati ya umati uliojitokeza.
Hata hivyo, idadi ya waliojitokeza asubuhi ilikuwa ni kubwa ukilinganisha na waliojitokeza mchana hali iliyowafanya wote waliofika kuanzia saa 7:00 mchana kuruhusiwa wote kuingia ambao hawakuzidi hata 20.