
Dodoma. Serikali imetangaza kuanza rasmi utekelezaji wa mwongozo wa kuwatambua na kutoa kipaumbele kwa wanaojitolea katika kazi mbalimbali, hasa pindi zinapotokea nafasi za ajira.
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Deus Sangu, aliliambia Bunge leo, Ijumaa Mei 2, 2025, kwamba mwongozo huo utaanza kutumika rasmi kuanzia Julai Mosi, 2025.
Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Saputu, ambaye aliuliza ni lini Serikali itakamilisha mwongozo wa kutoa kipaumbele katika ajira zinazotangazwa kwa wanaojitolea.
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alihoji ni kwa nini Serikali isitangaze mpango huo sambamba na malipo kwa vijana wanaojitolea.
Mbunge mwingine aliyeuliza swali la nyongeza ni Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, ambaye alihitaji kujua ni vipi Serikali itatoa kipaumbele kwa vijana wanaojitolea pindi nafasi za ajira zitakapojitokeza katika Utumishi wa Umma, kama ilivyoagizwa na Spika.
Naibu Waziri alijibu kwa kusema kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma (Volunteering Guidelines in Public Service), na kwamba utekelezaji wake utaanza hivi karibuni.
“Mwongozo huu umeandaliwa kwa kuzingatia maoni ya wadau muhimu, wakiwemo waajiri wote ndani ya Utumishi wa Umma, na utaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025,” amesema Naibu Waziri, Deus Sangu.
Sangu amesema kwamba Mwongozo huo unalenga kubainisha mambo muhimu ya kuzingatiwa na vijana wa kujitolea pamoja na taasisi za umma.
Aidha, unatoa fursa kwa vijana wa kujitolea kupata manufaa ya ziada, pamoja na kuwapa uzoefu na uwezo wa kushindana pindi nafasi za ajira zitakapojitokeza.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, lengo la mwongozo huo ni kukidhi matakwa ya Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008.
Kuhusu masuala ya malipo, amesema kuwa mwongozo huo umeelekeza kuwa vijana wanaojitolea waanze kulipwa angalau posho za kujikimu, ili kuwasaidia kukabiliana na mahitaji muhimu ya kila siku wanapotekeleza majukumu yao.