Wanaojipitisha majimboni kusaka ubunge CCM kushughulikiwa

Mtwara. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kuwaonya makada wanaojipitisha katika majimbo kabla ya wakati na kusababisha usumbufu kwa waliopo kwenye nafasi hizo, kikisema watachukuliwa hatua ikiwamo kukatwa.

Viongozi mbalimbali wa chama hicho wamekuwa wakitoa kauli za onyo na kuwatahadharisha wale wanaotaka kuwania nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kusubiri muda ufike.

Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama hicho waliowaonya wale walioanza kampeni mapema kwamba, watawachukuliwa hatua.

Jana, Jumamosi, Machi 1, 2025, Katibu wa Organizesheni wa chama hicho, Issa Ussi Gavu anaingia kwenye orodha ya viongozi waliotoa onyo kama hilo.

Gavu alitumia jukwaa la uzinduzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Newala mkoani Mtwara kuzungumza na mamia ya wanachama na wasio wanachama waliojitokeza, akisema atakayebainika kusumbua ufanyaji kazi wa wabunge na madiwani waliopo madarakani kabla ya muda atashughulikiwa.

“Hatukatazi kuwa na nia ya kugombea ubunge na udiwani, kwa sasa kaa nayo moyoni mpaka muda sahihi utakapofika utachukua fomu na kuomba ridhaa, ila kwa sasa tukikubaini tutakushughulikia,” amesema Gavu.

Gavu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amesema nafasi ambazo zimeshajazwa ni ugombea urais Tanzania na Zanzibar, nyingine zote zipo wazi.

Rais Samia amepitishwa kuwania urais. Dk Emmanuel Nchimbi akiwa mgombea mwenza huku Rais Hussein Ali Mwinyi akipitishwa kuwania urais Zanzibar.

“Ukiwa mtulivu ukaweka dhamira yako ya kugombea ukaiweka kwenye moyo wakati ukifika nenda kachukue fomu jina lako likirudi, tutawaomba ridhaa wanachama wenzako na sisi tutakupa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama chetu utuletee ushindi,” amesema.

Gavu amesema wakati ukifika na filimbi ikipulizwa kila mwanachama mwenye sifa ya kugombea kwa mujibu wa sheria za Tanzania na mujibu wa kanuni za CCM mtu huyo ataruhusiwa kuchukua fomu na kugombea.

“Lakini ukitaka kutumia njia ya mkato ukafanya vurugu au ukafanya ghasia zenye lengo la kuondoa utulivu, umoja na mshikamano wa chama chetu, tutahangaika na wewe,” ameonya.

“Wale wote wenye dhamira ya kutaka kugombea kwa tiketi ya CCM watajiandaa vizuri na mwaka huu 2025 kama tulivyowaletea wagombea wazuri katika nafasi za vitongoji na vijiji, tunahakikisha na watu wanaokuja kusimama kwa nafasi za udiwani na ubunge lazima wawe watu wenye kujitosheleza, sifa na uwezo wa kuwa viongozi.”

Alichokisema Dk Nchimbi

Dk Nchimbi alionya wanachama wanaotafuta uteuzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa njia zisizo halali huku akisema chama hakitasita kuwaengua watakaokiuka katiba, kanuni na maadili kuelekea uchaguzi huo.

“Tumeanza kuona matukio ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wagombea pekee.

“Wengine wanahamasisha vikao kutoa matamko kwamba wapitishwe bila kupingwa, wapo wanaoandaa kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za ndoa, lakini wahudhuriaji wanapewa posho na wamevaa sare za CCM ili ionekane kama mkutano wa kisiasa,” alisema Dk Nchimbi alipokuwa Dodoma.

 “Wapo wanaowapa posho wahudhuriaji wa mikutano wakiwa wamevaa sare za CCM ili kuonesha wanaungwa mkono. Tunawataka waache mara moja.”

“Wengine wameanzisha NGOs kwa malengo ya kisiasa, wengine wanatumia mbinu za kuwachafua waliopo madarakani kwa sasa.

“Kwa wote hawa, tunasema waache mara moja. Wanapoteza muda na kutufanya tufikirie kuwaengua.  Hatutavumilia mambo haya,” alionya.