
Dar es Salaam. Serikali imesema upelelezi katika kesi ya kusafirisha kilo 332 za heroini na Methamphetamine, inayowakabili washtakiwa tisa, upo hatua za mwisho kukamilika.
Wakili wa Serikali, Eva Kassa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Machi 6, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni mvuvi wa samaki Ally Ally(28), maarufu Kabaisa, Bilal Hafidhi (31) ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis (47) mvuvi wa samaki na Idrisa Mbona(33) ambaye ni muuza magari.
Wengine ni Rashid Rashid (24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji; Shabega Shabega (24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.
Pia, yupo Dunia Mkambilah (52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke; Mfanyabiashara Mussa Husein (35)mkazi wa Mwambani na Hamis Omary(25).
Wakili Kassa ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa shauri hilo upo hatua za mwisho kukamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.”
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 20, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hoteli ya White Sands, iliyopo Wilaya ya Kinondoni wanadaiwa kusafirisha kilo 100.83 za dawa aina ya Methamphetamine, kinyume cha sheria.
Shitaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za heroini, kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Aprili 22, 2024 wakikabiliwa na mashitaka hayo.