Wananchi watofautiana Jimbo la Ukonga kugawanywa

Dar es Salaam. Wananchi wa Ukonga wameonyesha mitazamo tofauti ya kugawanywa kwa jimbo la Ukonga ili kuwa na majimbo mawili, Ukonga na Kivule.

Mitazamo hiyo imekuja saa chache baada ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC) kueleza kuridhia mapendekezo ya kuligawa jimbo hilo.

Mapendekezo hayo yamepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wakazi wa Ukonga, wengine wakieleza ni wakati sahihi wa kuligawa jimbo hilo kutokana na ukubwa na wengine wakisema hakukuwa na sababu ya kuongeza gharama za kuwa na mbunge mwingine Kivule.

Leo Machi 24, 2025 Kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila imepokea na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Ilala (DCC) ya kuligawa jimbo hilo ili kuwepo na jimbo pendekezwa la Kivule.

Kwa mujibu wa Chalamila, mchakato unaofuata ni kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye mamlaka husika ikiwemo OR-Tamisemi ili kupata ridhaa.

Chalamila amesema jimbo jipya linalopendekezwa la Kivule litakua na kata sita ambazo ni Kipunguni, Mzinga, Msongola, Kitunda, Kivule na Majohe likiwa na watu 431,736 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022.

Jimbo la Ukonga litabaki na kata saba za Ukonga, Chanika, Gongo la Mboto, Zingiziwa Buyuni na Pugu Station likiwa na idadi ya watu 459,810.

Mapendekezo hayo yamepokelewa kwa mitazamo tofauti na wakazi wa Ukonga, baadhi wakieleza ni wakati sahihi wa kuligawa jimbo hilo na wengine wakisema kuwa na majimbo mawili ni kuongeza gharama, kwani mahitaji ya wananchi wa Ukonga si kugawanywa kwa jimbo.

Chiando Masatu wa Pugu Station amedai jimbo hilo ni kubwa kama tukiwa na wabunge wawili, hata huduma zitakuwa nyepesi, kuna maeneo huduma zilikuwa zinachelewa kufika kwa sababu ya  ukubwa wa jimbo hili, likigawanya itasaidia,” amesema.

Mjumbe wa Mtaa wa Pugu,  Farida Kilango amesema jimbo la Ukonga ni kubwa na ili utekelezaji ufanyike vema kwa wananchi ni vema ligawanywe.

“Likigawanywa na kuwepo wabunge wawili kila mmoja atashughulikia eneo lake, ingawa hivi sasa mambo yanashughulikiwa lakini likigawanywa litarahisisha mambo mengi kwa wananchi,” amesema.

Mathayo Venus wa Majohe amekuwa na mtazamo tofauti akibainisha takwa la wananchi si kuwa na mbunge mwingine, ni kuboreshewa huduma za kijamii.

“Sijui ni kwa namna gani tunakwenda kwenye ili, lakini kuongeza mbunge mwingine wa Kivule ni kuongeza gharama zisizokuwa na sababu, sisi hatuhitaji mbunge, tunahitaji miundombinu, zahanati, maji na huduma nyingine za jamii,” amesema Mathayo.

Nezia Nyalusi wa Kitunda amesema kugawanywa kwa jimbo hilo si suluhisho la wananchi kupata mtu wa kuwasemea bungeni.

“Huku ni kama kupeana nafasi za kipato tu, mbunge huyo wa Kivule atahitaji posho kwa miaka mitano, na gharama nyingine, bora hizo pesa zingeenda kufanya jambo jingine la maendeleo na tubaki na mbunge mmoja ambaye anawajibika,” amesema.

Februari 26, mwaka huu Tume Huru ya Taifa ya  Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi, ikiwa ni katika harakati za kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *