Wananchi wataka ushirikishwaji uboreshaji wa makazi

Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa programu ya kuboresha na kurejesha maeneo ya miji ambayo yameathiriwa na changamoto mbalimbali ukianza, wananchi wametaka kupewa elimu zaidi na kushirikishwa katika mchakato huo.

Hayo yameelezwa leo Aprili 4, 2025 na baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Makangira, kata ya Msasani jijini Dar es Salaam walipozungumza na Mwananchi baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Deogratius Ndejembi kutembelea eneo hilo na kufanya mkutano na wananchi.

Machi 25, 2025, Serikali ilibainisha maeneo 111 katika mikoa 24 yenye makazi duni na yanayoendelezwa kiholela nchini, ambayo yatafanyiwa maboresho kupitia upangaji upya wa miji, huku Serikali ikiahidi kushirikisha wananchi kwa karibu katika mchakato huo.

Hatua hiyo inatekelezwa chini ya Programu ya Uendelezaji wa Miji, inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Marekebisho hayo yanachochewa na ongezeko la idadi ya watu, kupungua kwa ardhi inayomilikiwa binafsi, upanuzi holela wa miji, ukosefu wa nyumba bora na za gharama nafuu, pamoja na lengo la kupunguza gharama za maisha.

Eneno la Makangira lenye wakazi takribani 5,247, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ni moja ya maeneo yanayotarajiwa kunufaika na mpango huo wa uboreshaji wa maeneo ya miji unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 4, 2025, Abdallah Hassan ambaye ni mkazi wa eneo hilo, amesema utekelezaji wa mradi huo utakwenda kuwasaidia kutatua changamoto za miundombinu zilizokuwa zikiwakabili hasa kipindi cha mvua kubwa.

Amesema kwa muda mrefu inapofika kipindi cha mvua eneo hilo linakuwa gumu kufikika kutokana na uchakavu wa miundombinu.

Hassan amesema kutokana na changamoto hiyo kuwepo kwa muda mrefu imewafanya baadhi ya watu kuuza maeneo yao na kwenda kuishi sehemu nyingine.

“Ukitokea msiba inakuwa mtihani hata unawekaje msiba na mtapitishaje mwili wa marehemu kutokana na namna mazingira yalivyo,” ameeleza.

Ameongeza kuwa hata mtu ni changamoto kumfikisha katika kituo cha afya kutokana na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki.

Amina Amiri, ameomba mamlaka husika kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi namna mradi utakavyotekelezwa, umuhimu wake na mchakato mzima kuwa shirikishi kwa wananchi.

“Tukijua umuhimu wa mradi huo kwetu utatusaidia hata kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wahusika wanaotekeleza bila ya kikwazo chochote,” amesema.

Hata hivyo, akizungumza na wakazi wa eneo hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Deogratius Ndejembi amesema wananchi watashirikishwa kwa karibu katika mchakato mzima wa utekelezaji wa mradi huo.

Katika kutekeleza hilo, Ndejembi ameagiza kuundwa kwa kamati ya wananchi wa eneo hilo yenye wajumbe wasiopungua tisa na wasiozidi saba.

Ametaka kamati hiyo izingatie usawa wa kijinsia pamoja na nafasi ya vijana ili kupata mawazo tofauti yatakayosaidia utekelezaji wa mradi huo kuwa wa ufanisi.

“Lengo ni kufanya utekelezaji wa mradi huo kuwa shirikishi na sio wataalamu na viongozi pekee,” amesema.

Amewasihi wakazi wa eneo hilo kuwa tayari kuwapokea wataalamu mbalimbali watakaofika kukusanya taarifa katika hatua za awali za utambuzi wa kila kaya.

Amewasisitiza wananchi wa eneo hilo kuwa hawatahamishwa katika eneo hilo hadi kipindi cha utekelezaji wa mradi, ambapo wananchi watapangishiwa nyumba katika maeneo mengine mpaka utakapokamilika.

“Baada ya kukamilika mtarudi katika maeneo yenu ambayo yatakuwa yameboresha na kuwa ya kisasa,” amesema.

Amewataka wananchi kuwa makini na watu watakaojifanya kutaka kuuziwa maeneo hayo baada ya kusikia kuna mradi wa uboreshaji wa makazi unakuja.

“Kuweni makini na watu hawa kwani nanyi mnastahili kupata makazi ya kisasa,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema lengo la programu hiyo ni kuboresha maisha ya makazi, kuboresha fursa za uchumi kwa wananchi na kufanya miji kuwa endelevu na eneo hilo.

Hivyo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mamlaka husika ili utekelezaji uweze kufanyika kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *