
Musoma. Wakati Tanzania na Kenya zinajiandaa kuadhimisha Siku ya Mto Mara, wakazi wa Mkoa wa Mara wanaoutegemea kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, wameomba mamlaka husika kuimarisha usimamizi wa rasilimali zake.
Wamesema lengo ni kuhakikisha utajiri huo wa asili unaendelea kuchangia usalama na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Septemba 9, 2024, baadhi ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka Mto Mara, wamesema licha ya jitihada zinazofanyika katika kuhifadhi mto huo, bado kuna changamoto kadhaa zinazoukabili na kutishia uendelevu wake.
Magige Jonathan, mkazi wa Kijiji cha Kwibuse wilayani Rorya amesema changamoto hizo ni pamoja na uvuvi haramu unaoathiri ikolojia ya mto huo.
Hivyo, amependekeza jitihada zaidi kuhakikisha Mto Mara unadumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Maisha yangu yote nimekuwa mvuvi na kwa kipindi cha nyuma samaki walikuwa wanapatikana kwa wingi, tulikuwa tunaishi kwa kutegemea uvuvi, ila siku za hivi karibuni samaki wameadimika. Hii ni kutokana na uvuvi wa kutumia zana zisizofaa,” amesema Magige.
Mkazi wa Kijiji cha Kirumi wilayani Rorya, Okoti Nyahende amesema mbali na zana haramu, pia shughuli za kibinadamu kando ya mto huo ni changamoto nyingine inayotishia uendelevu wake.
“Mara nyingi nyakati za maadhimisho tumekuwa tukishiriki kupanda miti kwa ajili ya kuhifadhi bonde la Mto Mara kwa ujumla, niombe jitihada ziendelee tusisubiri hadi maadhimisho yafike, mto huu pia ni chanzo cha uwepo wa tukio la uhamaji wanyama aina ya nyumbu katika hifadhi yetu ya Serengeti,” amesema Arodia Jackton.
Amesema matumizi ya rasilimali za maji ya Mto Mara yanahusisha shughuli za kilimo, uvuvi na matumizi mengine na endapo hakutakuwa na usimamizi mzuri kunaweza kusababisha matumizi yasiyo endelevu.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), zaidi ya wavuvi 100 waliokuwa wanajihusisha na uvuvi haramu katika mto huo walisalimisha zana haramu zaidi ya 530 walizokuwa wakitumia kufanya shughuli zao.
Mtafiti kutoka Tafiri, Dk Benedicto Kashindye amesema zana hizo zimesalimishwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kutokana na uwepo wa mradi wa usimamizi wa ardhi oevu katika bonde la Mto Mara unaotekelezwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na WWF pamoja na halmashauri zinazozunguka mto huo.
“Mradi wetu wa miaka mitatu unatekelezwa katika vijiji vinavyozunguka Mto Mara mkoani Mara, hadi sasa tumetumia zaidi ya Sh20 milioni kuwanunulia zana halali za uvuvi wale wote walioamua kusalimisha zana haramu walizokuwa wakitumi awali,” amesema Dk Kashindye.
Amesema katika mradi huo wamejikita kwenye utoaji wa elimu na kuhamasisha wote wenye zana haramu kuzisalamisha kwa hiari, kisha kuwapa zana halali na katika kipindi cha miaka miwili yapo mabadiliko makubwa yametokea, ingawa kuna upungufu wa bajeti ya kukidhi mahitaji ya wavuvi.
Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Mara, Ghati Kisyeri, amewataka wavuvi na wananchi wote kuwa wasimamizi na walinzi wa rasilimali zilipo ndani ya mto huo, ili uwe endelevu kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
“Mkoa umeanzisha operesheni maalumu kwa jina la operesheni fagia kwa wavuvi wote wanaojihusisha na shughuli za uvuvi haramu na itakuwa endelevu na kutekelezwa chini ya usimamizi wa viongozi wa wavuvi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na wataalamu wa sekta husika,” amesema Ghati.
Maadhimisho ya Siku ya Mara hufanyika Septemba 15 kila mwaka kwa kuzishirikisha nchi za Tanzania na Kenya na mwaka huu yatafanyika nchini Kenya katika Kaunti ya Narok.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dk Masinde Bwire amesema shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika wakati wa maadhimisho hayo ya 13, ikiwa ni pamoja na kongamano la wanasayansi kujadili kuhusu utunzaji wa bonde la Mto Mara litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ni wa pamoja tuhifadhi bonde la Mto Mara kwa baionuai endelevu na ustahimilivu wa tabianchi. Tunatarajia kuwa na wageni kutoka serikali zetu mbili, yaani Kenya na Tanzania pamoja na wadau kutoka taasisi na mashirka mbalimbali na kwenye kongamano la wanasayansi mnenaji mkuu atakuwa Profesa Plo Lumumba,” amesema Dk Bwire.