Wananchi wapewe elimu ya bima kujinasua na majanga

Wakulima takribani 195 wa mpunga wamefufua matumaini ya kuendelea na msimu mwingine wa kilimo, baada ya kupokea fidia ya Sh110.7 milioni kutokana na hasara waliyopata.

Wapo waliokuwa wamekata tamaa kuendelea na kilimo kwa msimu mpya na wapo waliokuwa wanapambana kuuza nyumba zao ili waweze kulipa mikopo au marejesho kutokana na kuingiza fedha zao kwenye kilimo hicho ambacho mazao yao yamesombwa na mafuriko.

Itakumbukwa mwaka huu wakulima wa Mbarali walikumbwa na mafuriko, lakini wenzao wa Shamba la Kapunga imekuwa neema baada ya kufidiwa na bima kiwango hicho cha fedha.

Kila mwaka Juni 28 huadhimishwa Siku ya Bima Duniani, ikiwa na lengo la kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia bima katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Bima wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Bghayo Sagware alipozungumza wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara, maarufu kama Sabasaba ya mwaka huu, bima za mali ndizo zinazoongoza kukatwa nchini kwa asilimia 12 ikilinganishwa na bima za maisha ambazo idadi ya watumiaji bado ni kidogo.

Aliweka bayana kuwa elimu zaidi inahitajika kutolewa ili Watanzania watumie huduma za bima ya maisha kutokana na manufaa yake kuwa ni makubwa.

Taarifa ya Tira inaonyesha kwamba sekta ya bima inakuwa kwa wastani wa asilimia 15 ambapo takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha ongezeko la idadi ya watumiaji wa bima iliyofikia milioni 12 ikilinganishwa na watumiaji milioni 6 kwa mwaka 2022.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa sekta ya bima inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia 1.99 kwa takwimu za mwaka 2023, huku matarajio ikiwa ni kuwezesha sekta ya bima kuchangia kwa asilimia 3 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2030.

Hoja yetu ya kuweka takwimu hizo ni kuonyesha namna inavyohitajika kwa wananchi kuhamasishwa na kupewa elimu zaidi kuhusu bima.

Wakulima wa Mbarali ni mfano tu wa namna ambavyo watu wakielimishwa na kuhimizwa kutumia bima, wataweza kuondokana na umasikini.

Yapo maeneo mengine muhimu ambayo yanahitaji kuwekewa msukumo watu kukata bima kwa ajili ya manufaa yao ya baadaye.

Eneo la bima ya maisha, biashara, elimu siyo maeneo ya kubezwa, ajali na mengineyo.

Inawezekana kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapa elimu, na hao waliokata bima wanapokuwa wamefikwa na jambo, bima zao zifanye bila kuwepo ubabaishaji.

Mathalan, tunaona sekta ya kilimo imeajiri watu wengi zaidi nchini, hiyo ni ishara taasisi mbalimbali za bima, benki zielekeze mikakati yao kuwawezesha wakulima ili waweze kuwa na uelewa kisha wakate bima ya shughuli zao za kilimo.

Pia hiyo ifanyike kwa wafanyakazi hata wa viwandani, migodini, na hata wale waliojiariji kwa shughuli zao binafsi.

Kundi jingine muhimu ambalo linahitaji msukumo ni wajasiriamali ambao wanayo fursa ya kukata bima kwa ajili ya shughuli wanazozifanya, hata kama ni kuweka kidogo kidogo.

Hivyo ni muhimu watu wakawa na uelewa kuhusu sera ya bima, vilevile mamlaka inayosimamia eneo la bima ipanue wigo wake katika kufikisha elimu ya bima na kupanua maeneo ambayo makundi yote yatafikiwa na huduma ya bima iwe mjini au vijini.

Kampuni na tasisi zinazoshughulika na bima ziendelee kuhimiza wananchi na wateja wao kuhusu umuhimu wa kutumia bima kama ilivyofanyika kwa wakulima wa Mbarali na matokeo wameyaona wenyewe.