Wananchi wa Malawi waandamana kulalamikia uhaba mkubwa wa petroli na dizeli

Polisi katika mji wa Lilongwe nchini Malawi leo Jumatatu wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati wa waandamanaji waliotaka kujiuzulu Waziri wa Nishati na Madini wa nchi hiyo kutokana na uhaba mkubwa wa mafuta ya petroli na dizeli katika miji mbalimbali ya nchi hiyo unaoendelea kwa muda wa mwezi mmoja sasa.

Waandamanaji walimiminika mitaani huku wakipiga nara dhidi ya serikali kueleza kukasirishwa na tatizo la ukosefu wa mafuta huko Malawi kwa muda wa mwezi mmoja. 

Hata hivyo, katika muda wa chini ya saa moja, maafisa wa polisi walikuwa tayari wamefika katikati ya mji mkuu Lilongwe ambapo walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. 

Takwa kuu la waandamanaji Malawi ni kujiuzulu Ibrahim Matola, Waziri wa Nishati na Madini wa nchi hiyo na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Malawi (MERA), Henry Kachaje kwa kushindwa kushughulikia tatizo la mafuta.

Kwa karibu mwezi mmoja, Malawi  inasumbuliwa na uhaba mkubwa wa mafuta ikiwa ni pamoja na petroli na dizeli ambao umedumaza huduma muhimu kama vile usafiri wa umma na hospitali, ambapo uzalishaji wa umeme unategemea mafuta, na hivyo kuzidisha mfadhaiko wa watu.