Morogoro. Wananchi wa Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wamesema upatikanaji wa maji safi na stakabadhi ghalani, barabara za ndani ni miongoni mwa kero zinazowasumbua, hivyo wamemuomba Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla kuingilia kati.
Waliwasilisha kero hizo leo Ijumaa Mei 16,2025 wakati aliposimama kuwasiliamia wananchi wa Dumila akielekea wilayani Gairo kuendelea na ziara ya kuimarisha chama hicho, sambamba na kupokea na kusikiliza kero za wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Katika maelezo yake, Mkazi wa Dumila Said Khatib amesema stakabadhi gharani inawaumiza wakulima wanaotakiwa kupeleka mazao yao gharani pasipo kuambiwa yatanunuliwa kwa kiasi gani.
“Changamoto yetu katika mazao ya ufuta na mbaazi tunaambiwa kuna stakabadhi gharani inatuumiza sana sisi, maana siku ya mnada ndio tunaambiwa bei, naomba hili jambo uliangalie kwa makini sana,” amesema Khatib

Mkazi mwingine, Shani Mwinyimvua amesema changamoto kubwa waliyonayo Dumila ni upatikanaji wa majisafi akisema sasa hivi wanatumia ya chumvi, akimuomba Makalla kuwasaidia kusukuma ajenda hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewajibu kuwa tatizo la maji sawa, lakini kuhusu stakabadhi ghalani, amewataka wenye shida kumuona moja kwa moja kwa ajili ya utatuzi.
Wakati huohuo, mbunge wa jimbo hilo, Profesa Palamagamba Kabudi aligusia kero za barabara za ndani za Dumila, ingawa aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa Serikali itazifanyia kazi.
Wa kwanza kujibu kero hizo, alikuwa Mkuu wa Mkoa Adam Malima aliyesema suala la barabara lipo kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), hivyo atalifikisha katika kamati ya barabara ya mkoa ambayo yeye ni mwenyekiti.
“Katika miji ya mkoa wa Morogoro inayokuwa kwa kasi ni Dumila, hili la barabara nitalichukua na nitaliweka katika utekelezaji ili fedha za mwakani zikipatikana iwekwe kwenye utaratibu ili kuipendezesha Dumila,” amesema.
Kuhusu suala la maji, Malima amesema atawaelekeza Wakala wa Usambazaji Maji na Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Morogoro ili kupima kiwango cha ubora wa maji na kuyafanyia tathimini.
“Hapa Dakawa tumebaini kuna vyanzo vyanzo vya visima vinavyotoa maji ambayo yanakusudiwa kwenda Morogoro Mjini. Ikiwa tumepima na kukosa vyanzo hapa Dumila, nitawaomba watu wa Ruwasa wayagawe maji ya Dakawa yaje hapa ili kuongeza upatikanaji wa huduma hii,” amesema.
Akijibu hoja ya stakabadhi ghalani, Malima amesema ukimuona mtu anatoka hadharani anazungumzia suala hilo, basi haelewi na ana shida nayo.
“Sifa yangu, na Morogoro wananijua, simung’unyi maneno, ukimuona mtu anaipinga hadharani ana shida nayo kwenye mambo mawili, mosi ni mchuuzi au haielewi.

“Juzi tumefanya kikao kikubwa Morogoro mjini nani anakataa kwamba stakabadhi gharani imetoa bei ya kakao kutoka Sh6,000 hadi 28,000 au ufuta ulikuwa Sh2,000 unakwenda Sh4,000,” amesema.
Mbali na hilo, Malima amesema kuna watu wanahujumu stakabadhi kuanzia chini hadi mfumo mzima, akiwataka wananchi wasema ukweli tatizo la mfumo ni lipi.
“Mimi ndio Mkuu wa Mkoa, wewe niambie tatizo la stakabadhi nimepeleka mzigo siku sita hatujapata fedha, hatukuambiwa bei ya soko. Ukiona vitu vyote hujaambiwa, ujue hapo kuna mtu ana jambo lake,” amesema Malima.
Alichojibu Makalla
Akichangia hoja hiyo, Makalla amesema mtu anayepinga stakabadhi ghalani na kujitokeza hadharani labda aseme fedha zinachelewa anaweza kueleweka, lakini si kuipinga.
“Nimetoka Lindi na Mtwara, ukiwaambia wasiuze korosho kwa stakabadhi ghalani hawakuelewi, kwa sababu wanafaidika na maisha ya watu yamebadilika. Uzuri wa stakabadhi gharani ni ushindani wa bei badala ya kupitia madalali.
“Mtu akianza kuipinga stakabadhi gharani tutamshangaa, lakini ikitokea mmeuza mazao yenu kisha fedha zimecheleweshwa hapa ndio viongozi wa wilaya na mikoa wanaingia ili watu walipwe,” amesema Makalla.
Makalla alivyokuwa Naibu wa Waziri wa Maji alikuwa akipata shida kila alivyofika Dumila kwa sababu asili ya eneo hilo ukichimba unakutana na asili ya chumvi.
“Alichokisema Malima kitasaidia njia nyingine kupata maji baridi. Palipo na changamoto lazima jitihada ziendelee, ndio maana Serikali kwa kutambua changamoto ya Dumila, inafanya jitihada za kuboresha upatikanaji wa maji.
“Niwaombe wananchi wa Dumila, hakuna mtatuzi wa changamoto zetu zaidi ya Serikali ya CCM. Mimi ni jirani yenu, Dumila ilikotoka ni mbali na ilipo sasa ni pazuri, tumezichukua na tutazifanyia kazi changamoto,” amesema Makalla.