Wananchi, Serikali wote wanao wajibu wa kuheshimu sheria Z’bar

Wiki iliyopita, Zanzibar iliadhimisha Siku ya Sheria, kama ilivyofanyika Tanzania Bara na katika mataifa mengi duniani. Maadhimisho haya ni muhimu kwa nchi kama Tanzania, ambayo katiba na sheria zake zinalenga kujenga utawala wa kidemokrasia unaozingatia haki na usawa kwa wote.

Siku hii ni wakati mwafaka wa kutathmini namna katiba inavyoheshimiwa na sheria zinafuatwa na kila taasisi na mtu binafsi, awe raia au mgeni. Katika maadhimisho hayo, tangu kufunguliwa na Rais Hussein Mwinyi hadi hitimisho lake, msisitizo mkubwa uliwekwa katika umuhimu wa kuheshimu sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa misingi ya usawa bila ubaguzi.

Kauli hizi zinatoa matumaini kwamba bado ipo dhamira ya kuzingatia katiba na sheria za nchi. Hata hivyo, maadhimisho haya pia yalipaswa kuwa fursa ya kuchunguza changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria na kupendekeza marekebisho yanayohitajika.

Ingawa Zanzibar ina katiba na sheria nzuri zinazolinda haki za wananchi, bado kuna malalamiko kuhusu utekelezaji wake.

Mojawapo ya changamoto kubwa ni kuhusu vitambulisho vya Mzanzibari, ambavyo ni haki ya kisheria kwa wananchi wa Zanzibar.

Hivi karibuni, uandikishaji wa vitambulisho ulifanyika katika Shule ya Sekondari ya Lumumba na Unguja, mamia ya watu walikaa siku tatu wakisubiri huduma bila mafanikio. Baadhi waliripotiwa kuzungushwa na hatimaye kukata tamaa, hali inayowafanya kuhisi kama wakimbizi katika nchi yao wenyewe.

Aidha, kuna wasiwasi kwamba hata waliopata vitambulisho huenda wakakosa haki ya kupiga kura. Hali hii ilionekana Wilaya ya Wete na Pemba ambako watu wengi hawakuandikishwa kwa sababu mbalimbali, yakiwamo matatizo ya mtandao na madai ya upendeleo wa kisiasa.

Matukio mengine yenye utata ni vifo vya watu waliokuwa chini ya ulinzi wa vyombo vya dola, vilivyoripotiwa miezi miwili iliyopita katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Ingawa kisheria uchunguzi wa kina unatakiwa kufanyika na matokeo yake kuwekwa wazi kwa umma, bado hakuna taarifa za wazi kuhusu hatua zilizochukuliwa.

Changamoto nyingine inahusiana na haki ya dhamana kwa watuhumiwa. Kisheria, dhamana ni haki ya msingi isipokuwa kwa makosa maalum yaliyoainishwa.

Hata hivyo, kumekuwa na matukio yanashindwa kutatuliwa kwa sababu ya masharti ya dhamana kuwa magumu na hayana uhalisia.

Mfano ni mtu kutakiwa kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari ili apate dhamana, ilhali alikuwa amenyimwa awali. Vilevile, masharti kama dhamana ya hati ya nyumba au mali isiyohamishika yanakwamisha watu wasiokuwa na rasilimali hizo.

Pia, ipo tabia ya baadhi ya viongozi na wale wanaojiona “watu wakubwa” kukataa kuitikia wito wa mahakama, jambo linalokiuka misingi ya utawala wa sheria. Hili limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu, lakini hakuna hatua dhahiri zinazochukuliwa.

Tatizo jingine ni kwamba wananchi wengi hawaelewi sheria zao kutokana na ukosefu wa elimu ya kisheria. Wawakilishi na wabunge, ambao ndio watunga sheria, hawafanyi juhudi za kuelimisha wananchi kuhusu sheria zilizopo au mpya zinazopendekezwa.

Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, wataalamu wa sheria walihusishwa katika mijadala ya shule za sekondari, wakielimisha wanafunzi kuhusu haki na wajibu wao kisheria. Mpango huu ulisaidia vijana kumaliza masomo yao wakiwa na uelewa wa sheria za nchi. Ni vyema mpango huu ukarejeshwa, kwani utasaidia kupunguza maonevu na ukiukwaji wa haki unaofanywa na wale wanaojiona wako juu ya sheria.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar yalipaswa kuwa fursa ya kuangazia changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki na kufanyiwa kazi kwa suluhisho la kudumu. Utekelezaji wa sheria kwa haki na usawa ndio msingi wa utawala bora.

Ni jukumu la kila mdau, kuanzia mahakimu, polisi, maofisa wa mashtaka, wanasiasa, na wananchi kwa ujumla, kuhakikisha kuwa sheria si nadharia tu, bali inatekelezwa kwa uhalisia ili kila mtu apate haki yake bila ubaguzi.