
Serengeti. Wakazi wa Kijiji cha Makundusi, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamelalamikia ongezeko la matukio ya wanyamapori, hususan tembo na simba kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kuvamia makazi yao na kusababisha uharibifu wa mali na kuwafanya waishi kwa wasiwasi.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kuangalia namna ya kusaidia kuondokana na changamoto hiyo ambayo wameeleza inatishia usalama wao na mali zao.
Malalamiko hayo yamewasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo jana, Aprili 17, 2025, huku wakidai kuwa kwa sasa simba wamesogea karibu zaidi na makazi yao na wengine wakijificha kwenye eneo lililotengwa kijijini hapo kwa ajili ya malisho.
“Mkuu wa Mkoa, hivi tunavyoongea kuna mwenzetu yupo hospitali baada ya kushambuliwa na simba juzi, na haya matukio yamekuwa yakitokea mara kwa mara. Tunaomba usaidizi wa Serikali ili kumaliza shida hii,” amesema mkazi wa kijiji hicho, Lucas Kosuri.
Kosuri amesema matukio ya wanyamapori kuvamia makazi kijijini hapo yameongezeka, hata hivyo hakutaja takwimu halisi. Ameeleza kwamba Serikali inapaswa kuingilia kati ili kuwanusuru wananchi hao.
Kwa upande wake, Mtuki Marwa amesema mbali na kujeruhi watu, wanyamapori hao pia wamekuwa wakivamia mifugo malishoni au kwenye zizi na kuwala, hivyo kuwasababishia hasara wafugaji.
Naye Owino Kagoro amesema:“Wanyama hawa wamekuwa wakivamia mashamba yetu pia, wanaharibu mazao. Hali hii inatishia usalama wa chakula katika kijiji chetu. Hatutaki kuwa ombaomba kwa sababu sisi ni wakulima na wafugaji. Serikali ifanye jambo kumaliza tatizo hili.”
Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, ametoa wiki mbili kwa Idara ya Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuanzisha kituo cha ufuatiliaji wa wanyama hao ili kuwadhibiti na kuepusha madhara yanayotokea.
Amesema Serikali haiwezi kukaa kimya wakati vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa vijiji hivyo, na kwamba lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti matukio hayo.
Amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia kuratibu na kushughulikia kwa haraka pale panapotokea tukio lolote la mnyama kuvamia kijiji, ili hatua zichukuliwe kwa wakati kabla madhara hayajawa makubwa.
“Ndani ya wiki mbili nataka kituo hicho kiwepo, na mhakikishe mnatoa taarifa muhimu kwa wananchi na kuwaelimisha jinsi ya kukitumia kituo hicho, ikiwa ni pamoja na kutoa namba za simu ambazo zitakuwa zinapokelewa kwa wakati na muda wowote pale wananchi watakapopiga kuomba msaada,” amesema.
Pia, ameagiza uongozi wa kijiji hicho pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuanza mara moja mchakato wa ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kiume wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Makundusi iliyopo kijijini hapo.
Amesema uwepo wa hosteli hiyo, mbali na kuboresha taaluma, pia utaimarisha usalama wa wanafunzi hao ambao wamekuwa wakilazimika kutembea kila siku kwenda na kurudi shule katika mazingira hatarishi.
“Nimeambiwa wanafunzi wa kiume wanasoma kutwa, na hapa kuna changamoto ya wanyama wakali ambao wanakatisha maeneo haya mara kwa mara. Hii ni hatari sana. Jambo hili lazima tulichukue kwa uzito wake. Serikali ya kijiji kupitia mapato yenu yatokanayo na maeneo ya jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori, anzisheni mchakato wa ujenzi wa bweni mara moja,” ameagiza.
Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan, amekiri kuwepo kwa vitendo vya wanyamapori kuvamia kijiji hicho mara kwa mara, huku akiahidi kutekeleza agizo hilo la Mkuu wa Mkoa la kuanzisha kituo hicho.
“Ni kweli hapa kuna changamoto ya uvamizi wa wanyama hasa simba na tembo. Kwa sasa sina takwimu, lakini wanyama hawa wamekuwa wakiharibu mali na kujeruhi. Tumekuwa tukishirikiana na wadau katika kukabiliana na hali hii,” amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Makundusi, Joseph Mseti, amesema kutokana na agizo hilo la mkuu wa mkoa, ujenzi wa hosteli hiyo utaanza Julai 2025 na kukamilika ndani ya miezi mitatu.