Wananchi Moshi walia mkandarasi kuelekeza maji katika makazi yao, wafunga barabara

Moshi. Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mabogini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia mkandarasi anayejenga barabara eneo la Spenconi kuelekeza mitaro ya maji katika maeneo yao hali inayosababisha mafuriko kwenye makazi yao.

Hali hiyo imesababisha leo Alhamisi, Aprili 17, 2025 wananchi hao kuifunga barabara ya Spenconi- Fonga Gate- Mabogini- Kahe, kwa zaidi ya saa tatu kushinikiza Serikali kuingilia kati ili mitaro ya barabara hiyo ielekezwe katika mto njoro na kuwaondolea athari wanazokutana nazo kwa sasa.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 31, kwa sasa mkandarasi anajenga kwa kiwango cha lami kilometa 1.2, kipande ambacho wananchi wanalalamikia mitaro ya maji kuelekezwa katika maeneo yao ya makazi.

Hatua hiyo imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava akiwa ameambatana na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Moshi na Bonde la Pangani kufika eneo hilo ili kuzungumza na wananchi na kufanya tathmini ya athari zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi hao, wamesema kipindi hiki cha mvua wanaishi kwa wasiwasi wakihofia usalama wao kutokana na mitaro inayopitisha maji ya mvua kuelekezwa kwenye maeneo yao.

Fatuma Omary, mkazi wa mabogini amesema mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Alhamisi Aprili 17, imewaathiri na kuwafanya washindwe kulala kutokana na maji kuingia katika makazi yao.

“Mtaro uliochimbwa Spenconi umeelekeza maji mtaa wetu, maji mengi yameingia ndani, yameharibu vitu vyetu, tunaiomba serikali itusaidie kwa sababu tunapata adha na familia, watoto hawalali na sisi hatulali, tuna wasiwasi na mvua zimetangazwa zinaendelea na sisi kwa sasa hatujui tuelekee wapi na siku ya leo hatujui tutalala wapi,” amesema Omary.

Juma Khatibu, mkazi wa mabogoni amesema:”Changamoto ya maji haya tumeshairipoti kwa sababu mitaro imeelekezwa kwenye makazi na kila anapoulizwa mkandarasi anatoa majibu mapesi huku wananchi wakiathirika.

Leo tumeona wananchi wametoka wamefunga barabara. Tuishauri serikali iangalie namna ya maji haya yaelekezwe mtoni ili kunusuru wananchi.”

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava akizungumza na wananchi katika eneo la Mabogini

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bogini Juu, Zuberi Bakari amesema kaya 30 katika kitongoji hicho zimeathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo.

“Chanzo barabara yetu inatengenezwa, mkandarasi alielekezwa mtaro anaotengeneza ufike kwenye Mto Njoro ili haya maji yaelekee huko lakini mkandarasi hajatekeleza hilo na wameziba sehemu maji yanapogawanyikia yasigawanyike yaende sehemu moja, hali ambayo inasababisha yaingie kwenye makazi ya watu,” amesema Bakari.

Alichokisema DC

Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Moshi (DC), Godfrey Mnzava amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maji yanayotoka maeneo ya milimani yameathiri ukanda wa bondeni ambapo baadhi ya wananchi wameathirika.

“Tunazo mvua ambazo zinaendelea kunyesha katika wilaya yetu ya Moshi na mvua hizi zimetuletea changamoto kwenye baadhi ya maeneo yetu kwa sababu maeneo ya bondeni yanapokea maji mengi sana kutoka maeneo ya milimani,” amesema Mnzava.

“Hapa kuna mambo mawili, jambo la kwanza wapo baadhi ya wananchi katika eneo la Spenconi asubuhi walifunga barabara. Wakati tunaendelea kutengeneza barabara hii kuna sehemu tumefunga maji yanayoingia kwenye ule mtaro kwa sababu bado ni mbichi na tunaendelea kutengeneza barabara,” amesema.

“Wananchi walidhani maji yale ambayo tumeyaelekeza kwenye mto njoro ndiyo ambayo yamekuja kuleta changamoto kwenye maeneo yao haya, lakini tumepita wote na wananchi tumeenda nao hadi kule chini tumeona maji yale siyo tu yanatokana na lile eneo ambalo tumefanya uchepushaji bali ni maji pia ambayo yanatoka maeneo ya  mlimani ambayo yamefurika kwenye mashamba na kuleta changamoto kwenye maeneo ya makazi.”

Mkuu huyo ametoa maelekezo kwa wataalamu kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ndani ya siku mbili kukamilisha ujenzi wa mfereji unaopeleka maji katika mto njoro, ili kupunguza athari wanazopata wananchi.

“Pia ipo changamoto ya maji kujaa kwenye mto njoro na kufurika kuingia kwenye makazi ya watu, tumepita tumeangalia athari na tunaendelea kufanya tathimini ili kuinua tuta ambalo litapakanisha kati ya wananchi na mto Njoro ili kupunguza athari na tunaamini tuta hilo litapunguza kwa kiasi kikubwa athari za maji kuingia katika makazi ya wananchi,” amesema DC Mnzava.

Aidha mkuu huyo ametumia pia nafasi hiyo, kuwataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka katika maeneo hayo katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.

“Tunaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi, wale ambao wanaishi katika maeneo hatarishi wasikae katika maeneo hayo, kwa sababu taarifa ambazo tumeendelea kuzipokea kutoka katika mamlaka ya hali ya hewa bado mvua zitaendelea kunyesha hivyo waendelee kuchukua tahadhari wakati serikali pia ikiendelea kuchukua hatua za haraka kupunguza athari hizo ambazo zinaweza kutokea kwenye maeneo yetu haya,” amesema.

Meneja Tarura Wilaya ya Moshi, Cuthbert Kwayu amesema maji yaliyofurika katika makazi ya wananchi yametokana na mto njoro kujaa na kufurika na kwamba hakuna mitaro ya maji iliyoelekezwa kwa wananchi.

“Tayari tumetembelea maeneo mbalimbali katika Wilaya yetu ya Moshi kuna mifereji ilikuwa imeziba lakini tumeisafisha na maji yanapita vizuri ikiwemo barabara ya Kiboriloni Shule, Barabara Shanty na nyingine, lakini bado tunaendelea kupitia na kufanya tathimini ili kuhakikisha katika kipindi hiki cha mvua barabara zote zinapitika vizuri,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *