Unguja. Wananchi milioni 2.72 wamefikiwa na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia huku migogoro 5,704 ikitatuliwa katika mikoa 25 nchini.
Kati ya hao wanawake ni milioni 1.3 na wanaume idadi hiyo hiyp ambao wamefikiwa ana kwa ana na kusikiliza mashauri yao huku maudhuhi mtandaoni yakitazamwa zaidi ya milioni 43.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini wakati wa kuzindua kampeni hiyo katika Kijiji cha Mtende Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Kwa mujibu wa Sagini, kupitia kampeni hiyo, migogoro 5,704 imetatuliwa na migogoro mingine zaidi ya 18,987 inaendelea katika hatua mbalimbali, kati ya 23,396 ya muda mrefu iliyokuwapo.
“Kampeni hii imeleta amani na kufanya shughuli mbalimbali za wananchi ziendelee kufanyika baada ya kutatuliwa changamoto zao hususani katika migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, ajira hivyo wananchi kupata utulivu,” amesema.
Akizindua kampeni hiyo kwa mkoa huo ambao ni wa mwisho Zanzibar, Dk Mwinyi amesema Serikali zote mbili zinafanya jitihada kuimarisha haki sawa ambayo ni msingi muhimu ya utawala bora na kampeni hiyo italeta mwamko kwa wananchi kufuatilia haki zao.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika kijiji cha Mtende Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema lengo ni kuwafikia wananchi ambao hawana uwezo kupata huduma hizo kwani msaada wa sheria ni nguzo muhimu katika utawala wa sheria na maendeleo endelevu katika jamii na taifa.
“Upatikanaji wa haki ni kichocheo muhimu cha kudumisha amani, mshikamano, na inapokosekana haki ndio penye mgogoro, ukatili wa kijinsia na migongano ya kifamilia na vinachangia sana kuathiri ustawi wa jamii,” amesema Dk Mwinyi
Amesema pamoja na kudumisha amani na utulivu, Serikali inaendelea kuimarisha Mahakama na taasisi zote zinazosimamia utoaji wa sheria.
Dk Mwinyi amesema kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mahakama za mikoa na wilaya kwa fedha za ndani ambapo zimejengwa mahakama saba, kati ya hizo tano za mikoa na mbili za wilaya.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuongeza rasilimali watu wenye sifa katika utendaji wa mahakama na kuongeza majaji kutoka wanane hadi 14.
“Utekelezaji wa mipango yote hii umelenga katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa haraka na misingi ya usawa pamoja na kuzisogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi,” amesema.
Amesema ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake bila kujali uwezo wake wa kifedha, rangi, dini au jinsia yake.
Amesema katika dunia ya sasa lazima kuweka mazingira ya kumsaidia mwananchi asiweze kuingia kwenye matatizo ya kisheria na kampeni hii italeta mwamko mkubwa wananchi kufahamu haki zao na kufuatilia hasa wale wanaoishi katika maeneo ya mbali na weye uwezo mdogo.
Katika msingi huo, amezitaka wizara zote zinazohusika na sheria kushirikiana kutafuta rasilimali fedha na nyenzo zingine zinazohitajika.
Pia, ameiagiza wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar, kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza huduma hiyo ili msaada wa kutoa huduma hiyo uwe endelevu na kwa kutumia mobile kliniki.
Amewataka wananchi kutumia vyema elimu hiyo ili iwe msaada wa baadaye huku akiwasihi kuacha muhali na kuchukua hatua.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema wananchi wanahitaji huduma hiyo kwa kiasi kikubwa na kutumia fursa hiyo wajitokeze kuwasilisha changamoto zao zipatiwe ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema kuna migogoro mingi inayowakumba wananchi wa mkoa huo ikiwemo ya ardhi na ndoa, hivyo kuja kwa kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi kupata haki zao.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Joseph Magazi amesema ni jambo la faraja juhudi hizo zinaungwa mkono na Serikali kuhakikisha haki inapatikana kwa wote hasa waliopo katika mazingira magumu.
Amesema utaratibu huo si tu ni hitaji la haki za binadamu, bali ni kiini cha utawala wa sheria na ni muhimu kuendeleza huduma hizi na kuwapo mfumo madhubuti kufuatilia mashauri yanayoibuliwa.
Rais huyo amesema ZLS inapendekeza kuwapo na mbinu muafaka katika kuwafikia wananchi Kwa kuwatumia viongozi wa dini, taasisi za Serikali na mitandao ya kijamii kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Pia, amependekeza kuwa na mfumo wa pamoja baina ya wadau wa sheria na Serikali katika kushughulikia mashauri.
“Ni muhimu kuwa na mpango wa kuendelea na huduma za ushauri mradi utakapofika mwisho, ZLS tupo tayari kuandaa mikakati,” amesema.
Kampeni hii ya miaka mitatu ilianza kutekelezwa Machi 2023 na inatarajiwa kukamilika Februari 2026 ikiwa imetengewa Sh6 bilioni na mpaka sasa imeshaendeshwa katika mikoa 25 ya Tanzania bara.