
Mashambulizi yaliyofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) huko kaskazini na mashariki mwa jimbo la Gezira nchini Sudan yametajwa na taasisi ya kieneo ya Gezira Conference kuwa ni mauaji ya halaiki.
Taasisi hiyo ya kiraia imesema, wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) Ijumaa iliyopita walivamia mji wa eneo la Al-Kamelin na kuanza kufyatua risasi kiholela kutoka kwenye majengo marefu. Takriban watu 50 waliuawa na mamia ya wengine walijeruhiwa.
Ripoti zinasema, katika mji wa Tamboul kaskazini mwa Gezira, wapiganaji wa RSF walivamia na kuua makumi ya raia na kuwafukuza maelfu ya wengine.
Makundi ya wenyeji yanasema mashambulizi hayo yanaonekana kuchochewa na hasira baada ya kamanda mkuu wa RSF kuasi na kuhamia upande wa jeshi la serikali ya Sudan. Abu Aqlah Keikel, mtawala mkuu wa jimbo la Gezira alijisalimisha kwa jeshi la Sudan mapema Oktoba. Keikel anatoka jimbo la Gezira.
Muungano wa Madaktari nchini Sudan umesema kuwa mashambulizi ya RSF yamegeuza maeneo ya mashariki mwa Gezira kuwa “eneo la vita vya kikatili.”
Vilevile umewatuhumu wapiganaji hao kuwa wamefanya uhalifu wa kingono, mashambulizi kwenye vituo vya afya na kuwalazimisha raia kuyahama makazi yao.