Wanajihadi waua takriban wanajeshi 11 nchini Nigeria

Wapiganaji wenye mfungamano na kundi la Islamic State wamewauwa takriban wanajeshi 11 katika shambulio kwenye kambi yao katika jimbo la Yobe, kaskazini mashariki mwa Nigeria, duru za kijeshi zimeliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Huku wanajeshi wengi wakiwa bado hawajapatikana, afisa mmoja ameonya kwamba huenda idadi ya waliouawa ikaongezeka.

Wapiganaji kutoka Jimbo la Afrika Magharibi la Islamic State (ISWAP) walishambulia kambi moja katika mji wa Buni Gari siku ya Ijumaa jioni, na kuua wanajeshi 11, vyanzo viwili vya jeshi vimesema.

Walichoma moto kambi moja baada ya mapigano makali, vyanzo hivyo imeongeza.

“Magaidi hao, waliokuwa wamepanda malori kadhaa yaliyokuwa na silaha nzito na  silaha za kurusha roketi (RPG), walishambulia kambi hiyo na kuichoma moto baada ya kuwaua wanajeshi 11,” afisa mmoja wa kijeshi amesema.

“Idadi ya waliouawa inaweza kuongezeka kwani wanajeshi wengi wamekosekana na hatima yao bado haijulikani,” afisa huyo wa kijeshi ameongeza.

Washambuliaji walikamata silaha kabla ya kuchoma moto kambi hiyo, wakiteketeza magari na majengo kadhaa ya kijeshi, kimesema chanzo cha pili cha jeshi, ambacho kimetoa idadi ya wanajeshi 11 waliouawa.

Maafisa wote wawili waliomba kutotajwa majina yao kwa vile hawakuwa na idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu tukio hilo.

Video za matokeo ya uvamizi huo, zilizotazamwa na mwandishi wa habari wa AFP, zinaonyesha mabaki ya gari la kijeshi na lori kadhaa za kijeshi zilizoteketea kwa moto.

Kambi ya Buni Gari, kilomita 60 kutoka Damaturu, mji mkuu wa Jimbo la Yobe, imeshambuliwa mara kadhaa na wanajihadi.

Uasi wao wa miaka 16 umeua zaidi ya watu 40,000 na kuwalazimu karibu milioni mbili kukimbia makazi yao kaskazini mashariki mwa nchi.

Kambi ya Buni Gari ni kambi ya nane kushambuliwa na wanajihadi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kulingana na hesabu ya AFP.

Tangu mwaka 2019, wanajeshi wanaopigana na wanajihadi wamefunga kambi ndogo za kijeshi na kuhamia katika kambi kubwa, zinazoitwa “kambi kuu,” ili kukabiliana na mashambulio.

Lakini wakosoaji wanasema mkakati huu umewaruhusu wanamgambo kutembea kwa uhuru zaidi katika maeneo ya mashambani na kuwafanya wasafiri kuwa hatarini zaidi kwa mashambulizi na utekaji nyara.

Siku ya Jumatatu, watu 26 waliuawa wakati gari lao lilipolipuka baada ya kukanyaga bomu la ardhini karibu na mji wa Rann, karibu na mpaka na Cameroon.

ISWAP imedai kuhusika na mlipuko huo.

ISWAP na hasimu wake Boko Haram hivi karibuni wameongeza mashambulizi dhidi ya maeneo ya kiraia na kijeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Zaidi ya raia 100 waliuawa katika mashambulizi ya wanamgambo mwezi Aprili.

Wakati wa ziara yake katika mji wa kaskazini wa Katsina siku ya Ijumaa, Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliahidi kuwapa sialaha za kisasa na bora zaidi wanajeshi ili kupambana na “matishio ya ugaidi, ujambazi na uasi ambao umeendelea kwa muda mrefu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *