Wanajeshi wasiopungua 12 wa Nigeria wauawa katika hujuma ya Boko Haram

Wanajeshi zaidi ya 12 wa Nigeria waliuliwa jana Jumanne katika mashambulizi kadhaa ya kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya kambi ya jeshi katika jimbo la Borno kaskazini mwa nchi hiyo.

Magaidi wa Boko Haram walivamia kambi ya jeshi la Nigeria katika mji wa Kareto katika eneo la Mobbar. 

Sauti kubwa za ufyatuaji risasi zilisikika katika kambi hiyo ya jeshi wakati pande mbili zilipofyatuliana risasi. Jeshi la Nigeria limesema kuwa magaidi ya Boko Haram walirejea tena katika kambi hiyo ya jeshi kutekeleza hujuma ambapo baadhi ya raia wa kawaida walipigwa risasi. 

Magaidi wa Boko Haram 

Mashambulizi ya jana ya Boko Haram dhidi ya kambi ya jeshi la Nigeria yalijiri ikiwa siku kadhaa baada ya magaidi hao kutekeleza mashambulizi mengine dhidi ya askari jeshi wa serikali na kuuwa wanajeshi kadhaa. 

Babagana Zulum, Gavana wa jimbo la Borno ametuma salamu za rambirambi kwa Jeshi la Nigeria kufuatia kuuawa askari wake. 

Nigeria imeathiriwa na mashambulizi ya kigaidi kwa miaka 14 sasa ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100,000 na kupelekea wengine milioni tatu kuyahama makazi yao.