Wanajeshi wa Burundi waondoka mashariki mwa Kongo huku waasi wa M23 wakipanua uwezo wao

Burundi inaondoa vikosi vyake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako walikuwa wakipigana dhidi ya waasi wa M23, duru nne zimesema siku ya Jumanne, ikiwa ni pigo kubwa kwa jeshi la Kongo wakati likijitahidi kuzima mashambulizi ya waasi hao.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Lakini msemaji wa jeshi la Burundi amepuuzilia mbali ripoti za kuondoka kwa jeshi hilo kuwa ni “uongo”, na amesema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba wanajeshi wa nchi yake “wanaendelea kutekeleza misheni yao katika maeneo yao ya uwajibikaji” nchini Kongo.

Kujiondoa kulikuja wakati ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikiwashutumu waasi wa M23 kwa kuwaua watoto mashariki mwa Kongo wakati wa harakati zao, hali ambayo imeshuhudia kundi hilo likiteka miji miwili mikubwa ya mashariki mwa nchi.

“Idadi ya malori yaliyobeba wanajeshi (wa Burundi) yaliwasili nchini humo tangu jana” kupitia kituo cha mpakani, afisa wa jeshi la Burundi amesema, akithibitisha taarifa zilizoelezwa na vyanzo viwili vya Umoja wa Mataifa na mwanadiplomasia wa Kiafrika.

Wanajeshi wa Burundi walipigana pamoja na wanajeshi wa kongo, FARDC, kujaribu kuilinda Kavumu,kuankopatikana uwanja wa ndege unaohudumia Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, ulioanguka mwishoni mwa juma. Ilikuwa ni tuzo muhimu zaidi ya waasi tangu walipouteka mji wa Goma, jiji kubwa zaidi mashariki mwa Kongo, mwishoni mwa mwezi wa Januari.

Burundi imekuwa na wanajeshi mashariki mwa Kongo kwa miaka kadhaa, awali kuwasaka waasi wa Burundi wanaoendesha harakati zao mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka wake, lakini hivi karibuni, kusaidia katika vita dhidi ya waasi wa M23.

Kundi la M23 lililo na vifaa vya kutosha ndilo la hivi punde zaidi katika msururu mrefu wa vuguvugu la waasi wanaoongozwa na Watutsi kuibuka mashariki mwa Kongo.

Katika maandamano yao huko kusini, waasi siku ya Jumanne waliingia katika mji wa Kamanyola, kilomita 50 (maili 31) kusini mwa Bukavu, kulingana na wakazi wawili na chanzo cha M23. Msemaji wa jeshi la Kongo hakujibu mara moja maombi ya maoni yake.

Mapigano kati ya waasi na jeshi la Kongo pia yaliripotiwa siku ya Jumanne katika eneo la Lubero, kaskazini mwa Goma, afisa wa eneo hilo Kambale Vighuliro na kanali wa jeshi Alain Kiwewa wameliambia shirika la habari la REUTERS.

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi alikutana na mwenzake wa Angola Joao Lourenço mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, kujadili kuzorota kwa kasi kwa hali ya usalama mashariki mwa Kongo, ofisi ya rais wa Angola imesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.