
Takriban wanajeshi 600 wa Korea Kaskazini wameuawa wakipigana pamoja na vikosi vya Urusi katika vita vyao dhidi ya Ukraine, mbunge na mtaalamu wa kijasusi wa Korea Kusini amesema Jumatano.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Hadi sasa, hasara ya wanajeshi wa Korea Kaskazini inakadiriwa kuwa karibu 4,700, ikiwa ni pamoja na karibu vifo 600,” mbunge Lee Seong-kweun, mjumbe wa kamati ya kijasusi ya bunge, amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano mfupi wa Idara ya ujasusi ya Korea Kusini.
Korea Kaskazini ilikiri kwa mara ya kwanza wiki hii kwamba ilituma wanajeshi wake nchini Urusi kuisaidia kuchukua tena maeneo ya jimbo la Kursk la Urusi kutoka mikononi mwa wanajeshi wa Ukraine.
Takriban wanajeshi 2,000 waliojeruhiwa walirejeshwa nchini Korea Kaskazini kati ya mwezi Januari na Machi kwa ndege na treni, na wanaripotiwa kuzuiliwa huko Pyongyang na maeneo mengine ya nchi, Lee Seong-kweun amesema. Kuhusu waliofariki, miili yao ilichomwa nchini Urusi na majivu yao kurejeshwa Korea Kaskazini, amesema.
“Korea Kaskazini imeunga mkono Urusi kurejesha himaya yake kwa jimbo la Kursk kwa kupeleka wanajeshi 18,000 katika awamu mbili. “Tangu mwezi Machi, wakati Kursk iliporejeshwa kwa ufanisi, idadi ya mapigano imepungua,” Mbunge huyo ameelezea. Kulingana naye, “uwezekano wa awamu ya tatu hauwezi kutengwa kabisa,” ingawa Pyongyang bado haijatoa ishara yoyote mpya ya kutuma askari nchini Urusi.
“Kuboresha” uwezo wa kupambana
“Miezi sita baada ya majeshi ya Korea Kaskazini kuingia vitani, uwezo wao wa kivita unakadiriwa kuimarika kwa kiasi kikubwa, kwani uzoefu wao wa awali umepungua na wamekuwa mahiri katika kutumia mifumo mipya ya silaha, zikiwemo ndege zisizo na rubani,” mbunge huyo wa Korea Kusini ameongeza. “Hata hivyo, kutokana na kupelekwa kwa jeshi hilo kwa muda mrefu, kumekuwa na taarifa za utovu wa nidhamu miongoni mwa vikosi vya Korea Kaskazini, ikiwamo ulevi wa kupindukia na wizi,” amesema.
Wanajeshi waliotumwa Urusi, wanaoaminika kuwa vikosi maalum, waliamriwa kujiua badala ya kuchukuliwa wafungwa, Seoul ilisema hapo awali.