
Arusha. Wanahisa wa Benki ya CRDB Plc wameidhinisha kwa kauli moja gawio la jumla la Sh170 bilioni, ambalo ni kubwa zaidi kuwahi kutolewa na benki hiyo.
Hilo limejiri katika mkutano mkuu wa mwaka wa 30 (AGM) uliofanyika jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
Gawio hilo linaloidhinishwa lina maana ya Sh65 kwa kila hisa kwa wanahisa wa benki hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), likiwa ni matokeo ya mafanikio makubwa yaliyotokana na ongezeko kubwa la faida katika mwaka wa fedha wa 2024.
Hili ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na Sh130.6 bilioni zilizotolewa kwa wanahisa mwaka uliopita, likiendeleza mwenendo mzuri wa mafanikio ulioanza na Sh57.5 bilioni mwaka 2020.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay, ameelezea safari ya miongo mitatu ya benki hiyo kama “ya kuvutia,” akibainisha kuwa gawio hilo la kihistoria ni ishara ya uimara wa kifedha na pia ni ishara ya kuthamini wanahisa.
“Katika kusherehekea miaka 30 ya ubora wa huduma za kibenki, gawio hili la kihistoria si tu ni ushahidi wa uimara wetu wa kifedha, bali pia ni ishara ya shukrani kwa wanahisa wetu waliokuwa nasi katika safari ya mabadiliko, ubunifu na ukuaji,” amesema Dk Laay, ambaye amekamilisha kipindi chake cha uongozi kama mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo.
Faida baada ya kodi ya Benki ya CRDB ilipanda kwa asilimia 30 na kufikia Sh551 bilioni mwaka 2024, huku kampuni tanzu za benki hiyo zikichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kundi zima, kwa kuchangia asilimia sita ya faida yote baada ya kodi.
CRDB Bank Burundi ilipata faida baada ya kodi ya Sh40.3 bilioni, wakati CRDB Insurance, ambayo ndiyo mwaka wake wa kwanza wa uendeshaji, ilipata faida ya Sh343 milioni baada ya kodi. Kwa upande wa CRDB Bank DRC, benki hiyo inaendelea kukuwa kwa kasi na inatarajiwa kuanza kutengeneza faida kabla ya muda uliopangwa awali.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kundi na Mtendaji Mkuu wa Benki, Abdulmajid Nsekela, ameihusisha mafanikio hayo na dhamira ya benki hiyo ya kujumuisha watu wengi zaidi katika mfumo wa kifedha, mabadiliko ya kidijitali na upanuzi wa kanda.
“Tunapoadhimisha miongo mitatu ya kuwezesha jamii na kujenga mustakabali, matokeo ya mwaka 2024 yanathibitisha kuwa mbele yetu kuna mafanikio zaidi. Safari ijayo inalenga ujumuishaji wa kina, mabadiliko ya kidijitali, na mchango mkubwa katika kanda,” amesema Nsekela.
Aidha, mwaka 2024, jumla ya mali za Benki ya CRDB ziliongezeka kwa asilimia 25.3 na kufikia Sh16.7 trilioni, ongezeko hilo likichochewa zaidi na ongezeko la kitabu cha mikopo kwa asilimia 22.7 na kufikia Sh10.4 trilioni.
Benki iliendelea kujikita katika ujumuishaji wa huduma za kifedha kwa kuanzisha bidhaa kama akaunti ya Sadaka na mikopo midogo kupitia ushirikiano wa kidijitali ili kuwafikia watu walioko pembezoni.
Nsekela pia ameeleza ushiriki wa benki hiyo katika miradi mikubwa ya kikanda, ikiwemo uwekezaji wa viwanda vya grafiti kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (DBSA) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Afrika Kusini (IDC), hatua inayoiweka CRDB kama mdau muhimu katika uongezaji thamani na uendelezaji wa viwanda ndani ya Afrika Mashariki na Kati.
Kadhalika, ufanisi wa uendeshaji wa CRDB uliimarika kwa kupunguza uwiano wa gharama na mapato hadi asilimia 45.7, huku mikopo chechefu (NPLs) ikibaki kuwa ya chini kwa asilimia 2.9, hali inayoonyesha udhibiti mzuri wa gharama na nidhamu madhubuti ya mikopo.
“Maadhimisho haya ya miaka 30 ni hatua ya kihistoria. Dhamira yetu haijabadilika: kuwa taasisi ya kifedha inayotegemewa, yenye mchango chanya na iliyo tayari kwa mustakabali kwa vizazi vijavyo,” amesema Nsekela.