Wanafunzi zaidi ya 30 Same wanusurika kifo

Same. Zaidi ya wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari Tumaini Jema, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro,  wamenusurika kifo,  baada ya darasa waliokuwa wakisomea kuanguka kufuatia upepo mkali.

Pamoja na wanafunzi hao, mwalimu aliyekuwa katika darasa hilo naye alijeruhiwa katika tukio hilo, ambapo kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Same kwa matibabu zaidi.

Kufuatia tukio hilo ambalo limetokea Februari 25, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Same,  Kasilda Mgeni ameagiza kusitishwa  kwa masomo kwa  siku,  saba katika shule hiyo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.

Mkuu huyo ambaye aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama kwenda shuleni hapo, ameliagiza Jeshi la Polisi, Taasisi ya kupambana na Rushwa (Takukuru), pamoja na wataalam wa ujenzi wa halmashauri hiyo  kufanya uchunguzi wa kina kuhusu  tukio hilo pamoja na kukagua ubora wa majengo ya shule hiyo.

“Naagiza shughuli zote za masomo zisitishwe hapa shuleni ili kupisha uchunguzi wa kina kuhusu ubora wa majengo haya. Naomba vyombo vya usalama mfanye kazi yenu na mniletee taarifa ya nini ambacho kimetokea, ili tujiridhishe na usalama wa majengo haya,”amesema DC Kasilda.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo akimjulia hali mmoja wa wanafunzi ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same, baada ya kuangukiwa na jengo la darasa walilokuwa wakisomea.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya   aliwatembelea  wanafunzi hao pamoja na mwalimu, huku akisema hali zao zimeimarika.

Akizungumzia hali za majeruhi hao, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dk Alex Alexandra amesema waliojeruhuwa katika ajali hiyo ni wanafunzi 31, ambapo wasichana ni 14 na wavulana 17 na hali zao zinaendelea vizuri.

“Jana mchana tulipokea majeruhi 31, wavulana 17 na wa wa kike 14, katika hawa majeruhi hakuna  aliye katika hali mbaya, wote wanaendelea vizuri na afya zao zimeimarika,”

Dk Alexandra, amesema kutokana afya za wanafunzi hao kuendelea kuimarika,  muda wowote wanaweza kuruhusiwa hospitalini hapo.