Na Gideon Gregory, Dodoma
Wanafunzi, wazazi na walezi wamekumbushwa kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au Kozi.
Ushauri huo umetolewa leo Aprili 2,2025 hapa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wahitimu wa kidato cha Nne 2024 kufanya mabadiliko ya tahasusi za kidato cha Tano na kozi za vyuo ambapo zoezi hilo limeanza rasmi Machi 31, 2025 hadi Aprili 30, 2025.
“Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi/ walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa,”amesema.
Waziri Mchengerwa amesema ni muhimu wazingatie muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa, baada ya matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa, Ofisi haitashughulikia changamoto hizo kwa kuwa fursa ya kufanya mabadiliko hayo imeshatolewa.
Aidha, amesema kuwa TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari wa mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kuwawezesha kusoma tahasusi au kozi itakayowaandaa kupata utaalamu stahiki kwa maisha yao ya baadaye.
Mchengerwa ameongeza kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa mchakato huu, wahitimu wote wanahimizwa kufanya marekebisho ya machaguo yao ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS), unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
Waziri Mchengerwa pia amesisitiza kuwa huduma hiyo ya kubadilisha tahasusi ni bure, na iwapo wanafunzi watakumbana na changamoto, wanapaswa kuwasiliana na Dawati la Huduma kwa Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kupiga simu kwa namba +255 262 160 210 na +255 735 160 210.
The post WANAFUNZI, WAZAZI NA WALEZI SHAURIANENI KABLA YA KUFANYA MABADILIKO YA TAHASUSI/ KOZI – MCHENGERWA appeared first on Mzalendo.