Wanafunzi wanufaika wa Tasaf ‘walilia’ mikopo asilimia 100

Unguja. Wanafunzi wanaopata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wameiomba Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) kuwapatia mikopo kwa asilimia 100 ili kuwawezesha kumudu gharama za masomo na maisha.

Licha ya kupongeza hatua ya kunufaika na mikopo hiyo, wanafunzi hao wamesema bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali kwani familia zao hazina uwezo kugharamia kiasi kinachobaki.

Wakizungumza katika maonyesho ya maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo Februari 11, 2025 katika viwanja vya Kisonge Unguja, Zanzibar baadhi ya wanafunzi hao wamesema wanapata mikopo kwa asilimia tofauti kati ya asilimia 50 hadi 62 hivyo kuomba waangaliwe kwa jichop la pekee.

“Mimi nimeanza kunuafaika na Tasaf nikiwa darasa la tano mpaka sasa nipo chuoni, tumepata mikopo kupitia kaya masikini, tumesaidika kwani wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunisomesha,” amesema Rashid Ali Abdalla, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).

Hata hivyo, Rashid ambaye anasoma kozi ya utalii na utawala wa masoko na kupata asilimia 50, amesema licha ya mchango huo lakini kulingana na kiasi wanachokipata wanashindwa kumudu gharama zote za mahitaji na kuomba bodi iwaangalie kwa jicho la kipekee waweze kusoma bila changamoto.

Naye Il-Kham Ali Abdalla mwanafunzi wa mwaka wa kwanza fani ya Uhasibu na Fedha Suza, amesema wanashukuru kwa kupewa kipaumbele wanufaika wa Tasaf katika kupewa mikopo.

“Tunaiomba Serikali kupitia bodi ya mikopo ituwekee angalau asilimia 100 kwasababu kile kiasi kinachobaki bado familia zetu hazimudu kulipa,” amesema Il-Kham ambaye anapata mkopo kwa asilimia 62.

Rashid Ali Abdalla mwanafunzi wa Chuo Cha Taifa Zanzibar (Suza) akizungumza katika maonyesho ya maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo Tanzania viwanja vya Kisonge Unguja.

Mwanafunzi mwingine Mtumwa Ali Hija kutoka shehia ya Chaani Masingini ambaye amenufaikaa na Tasaf tangu darasa la sita hadi sasa akiwa chuo kikuu, amesema kusingekuwa na mfuko huo asingesoma akikumbushia jinsi alipofaulu masomo ya kidato cha nne lakini wazazi wake wakamwambia atafute kazi ya kufanya maana hawana uwezo kumsomesha.

“Nakumbuka nilipofaulu kidato cha nne niliambiwa na wazazi hawana uwezo kunisomesha kwa hiyo nitafute kazi nikafanye iliniuma lakini baadaye ndio mfuko ukanisaidia, nimesomeshwa hadi leo nipo chuo kikuu, japo kiwango tunachopata hakitoshelezi mahitaji, tunaomba kuongezewa,” amesema.

Ofisa ufuatiliaji kutoka Tasaf, Ramadhan Madari amesema wanapongeza bodi kukubali ombi la kuwapatia mikopo wanafunzi wanaotoka kaya masikini wapate mikopo asilimia kubwa ingawa bado wanasema fedha wanazopata haziwatoshi.

“Ukienda vijijini wazee wanashindwa kumudu gharama hizi na wengine wanatoka kijijini unakuta mwanafunzi anapewa Sh600,000 kwa muhula mmoja kwa hiyo anatakiwa aongezee Sh400,000 hawana uweze ni kaya masikini hali inakuwa ngumu,” amesema.

“Kwahiyo ni kweli kama kuna uwezekano vijana hawa wapewe asilimia 100 ukizingatia wanatoka kwenye kaya masikini na ni kweli masikini hazina uwezo,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Madari amesema:“Hii wiki ni ya mitihani, kwa siku mbili nyuma nimepokea maombi mengi ya wanafunzi wanataka tuwadhamini angalau wafanye mitihani familia zimekosa, bodi imelipia tayari lakini mzazi anashindwa kumalizia kinachobaki.”

Meneja Utawala Bodi ya Mikopo, Claud Casmir amekiri kuwapo na upungufu wa fedha licha ya wanuafaika wa Tasaf kupewa kipaumbele cha mikopo japo zinajitokeza changamoto za hapa na pele ikiwemo kiwango kidogo cha fedha.

“Bodi ya mikopo kuadhimisha miaka hii 20 lengo kubwa ni kuangalia namna gani tunaweza kupata vyanzo vingine vya fedha mfuko uweze kuwa mkubwa ili wenye mahitaji wapate, hata hawa wa Tasaf wapate asilimia asilimia 100,” amesema.