Geita. Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Geita umewataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani humo kuvunja ukimya, na kutoa taarifa mapema pindi wanapofanyiwa au kuona wenzao wakifanyiwa ukatili.
la kufanya hivyo ni kukomeshwa kwa vitendo hivyo kabla madhara hayajaongezeka.
Polisi hao wametoa wito huo kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa wanafunzi wa shule ya wasichana Geita, ikiwa ni moja ya shughuli wanazozifanya kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake.
Akizungumzia ukatili, Kaimu Mwenyekiti wa mtandao huo, Grace Kaijage amesema ni muhimu waathirika wa ukatili wakatoa taarifa mapema, ili kupata msaada wa matibabu na wa kisheria.
Kaijage amesema pindi taarifa zinapotolewa mapema humsaidia muhusika kupata msaada wa kisheria na ushauri wa kisaikolojia kwa haraka.
Amesema husaidia ushahidi kuthibitisha kosa kwani wataweza kukusanya ushahidi muhimu, kama vipimo vya kitabibu na maelezo ya tukio ambavyo vinaweza kusaidia katika hatua za kisheria.
“Msiogope kutoa taarifa pindi mnapofanyiwa au kuona mtu anafanyiwa vitendo vya ukatili, pia muwe tayari kutoa ushahidi ili wahusika wachukuliwe hatua,” amesema Kaijage.
Kaijage amesema moja ya changamoto kubwa katika kesi za ukatili ni kukosekana kwa ushahidi, jambo ambalo husababisha waathiriwa wengi kutopata haki.
“Taarifa zinapofichwa, wahusika huendelea kuwaumiza wengine, ni muhimu kupaza sauti mapema ili kusaidia kukomesha vitendo hivi,” amesema.

Askari wa Mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Geita wakifurahia na wanafunzi wa shule ya Wasichana Geita walipofika shuleni hapo kutoa elimu ya kupinga ukatili pamoja na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi
Mtandao wa Polisi Wanawake mbali na kutoa elimu ya kupinga ukatili pia wamegawa taulo za kike kwa wanafunzi ili ziweze kuwasaidia kujistiri wawapo shuleni.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda amewataka wanafunzi waliopata elimu, kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuripoti matukio yanayotokea katika jamii zao badala ya kunyamaza.
Bila kutaja idadi au aina ya ukatili unaofanywa shuleni, Beda amesema huko hali si nzuri kwani matukio mengi ya ukatili bado yanaendelea kutokea, hivyo ni wajibu wao kutoa taarifa mapema ili wasiharibu ushahidi.

Katibu Tawala Wilaya ya Geita Lucy Beda akizungumza na wanafunzi wa shule ya Wasichana Geita wakati Mtandao wa polisi wanawake walipofika shuleni hapo kutoa elimu ya ukatili na kugawa taulo za kike kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake.
“Hali si nzuri, yapo matukio mengi ya ukatili shuleni na majumbani. Msinyamaze, toeni taarifa mara moja, hii itasaidia wahusika kuchukuliwa hatua na kuzuia madhara zaidi,” amesema.