
Mwanza. Zaidi ya wanafunzi 400 wa shule za sekondari mkoani Mwanza wameelimishwa kuhusu faida za uwekezaji kwenye masoko ya mitaji, kuwa ni pamoja na kujiwekea akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Pia, wamefundishwa kwamba uwekezaji huo ni kwa mtu yoyote aliyefikisha umri wa miaka 18 na kiasi kinachotakiwa ni kuanzia Sh10,000 na kuendelea, na siyo lazima kuwa na fedha nyingi kama wengi walivyokuwa wanadhani.
Elimu hiyo kuhusu faida za uwekezaji kwenye masoko ya mitaji, imetolewa leo Februari 14, 2025 jijini Mwanza na Taasisi ya Uwekezaji ya UTT AMIS, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu Juu (HESLB), yaliyoanza Februari 10, 2025 na kumalizika leo.
Akieleza kuhusu faida hizo, Mkuu wa UTT AMIS tawi la Mwanza, Ligwa Temela amesema wamewafundisha kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye ili kuanzisha biashara zao baada ya kumaliza vyuo vikuu.
Temela amesema mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 55 anaweza kuwekeza kuanzia Sh10, 000 kwenye akaunti ya UTT Amis na kuendelea.
Amesema taasisi hiyo ya uwekezaji ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha na kuratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA), ilizinduliwa Desemba mosi, 2020 jijini Mwanza ili kuhudumia wawekezaji wenye mitaji mikubwa, ya kati na midogo wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Katika siku hizi tano, tumetoa elimu ya uwekezaji kwa wanafunzi zaidi ya 400, pia tumewafikia wananchi zaidi ya 50 waliosaini kwenye kitabu chetu cha mahudhurio. Lengo ni kuwapa uelewa na faida za kuwekeza UTT AMIS,” amesema Temela.
Awali, Temela alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kuwa taasisi hiyo ina jumla ya mifuko sita ukiwemo wa Ukwasi, Hatifungani, Umoja, Watoto, Kujikimu na Wekeza Maisha.
Mtanda ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwawezesha wananchi kujiwekea akiba pamoja na kuwekeza kwenye masoko ya mitaji.
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mirongo, Judith Habibu amesema amepata uelewa kuwa kuwekeza hakuhitaji kiasi kikubwa cha fedha kama wengi wanavyodhani, bali uthubutu na kujiwekea malengo.
“Mfano, wazazi wengi wamekuwa wakihangaika na ulipaji ada kipindi cha Januari, nimejifunza kumbe wanaweza kuwekeza kuanzia Sh10, 000 kwenye mfuko wa watoto kwa ajili ya kulipa ada za masomo ya watoto wao kipindi hicho kikifika,” amesema Judith.