Wanafunzi wa Kiyahudi waandamana London kumuunga mkono Ripota wa Umoja wa Mataifa, Albanese

Wanafunzi wa Kiyahudi wamefanya maandamano mbele ya Shule ya Mafunzo ya Mashariki na Afrika katika Chuo Kikuu cha London wakitangaza uungaji mkono wao kwa Ripota wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika maeneo ya Palestina, Francesca Albanese.

Albanese anajulikana kwa misimamo yake ya kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, ambayo yameua shahidi makumi ya maelfu ya raia na kusababisha janga kubwa la binadamu ambalo halijawahi kushuhudiwa.

Mnamo Novemba 5, Albanese alisema: “Kinachotokea Gaza kama kuwatesa watu kwa njaa kimfumo kwa lengo la uharibifu sio vita, bali kinapaswa kuitwa mauaji ya kimbari.”

Wanafunzi wa Kiyahudi wanaotangaza mshikamano wao na Palestina walikusanyika mbele ya jengo la Chuo Kikuu cha London kumuunga mkono Francesca Albanese na kupinga maandamano yaliyofanywa na kundi linalojiita “Kampeni ya Kupinga Chuki dhidi ya Uyahudi.” 

Maandamano ya wanafunzi wa Kiyahudi

Waandamanaji hao walikuwa wakipiga nara kama vile “Palestine Huru,” “Komesha Mauaji ya Kimbari,” na “Hakuna Amani Bila uadilifu.”