Madhara ya mzozo unaoendelea nchini DRC yanaendelea kushuhudiwa hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo, ambapo wanafunzi wakongomani wanaosoma nchini Kenya wanasema wanatatizika kisaikolojia na pia kifedha kutokana na ukosefu wa huduma za benki nyumbani.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Katika eneo la Juja, takribani kilomita thelathini na tatu kutoka jiji kuu la Nairobi, nakutana na kundi la wanafunzi kutoka DRC wanaosomea katika chuo kikuu cha JKUAT
Laurent Bujirike, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza ananielezea jinsi kukatwa kwa huduma za kutuma na kupokea pesa nyumbani kwao Bukavu, kumemwathiri.
‘‘Huwa nalipa kodi ya nyumba kabla ya tarehe tano ila mwezi huu nilichelewa na hata wenye nyumba wakawa wameanza kunitatiza.’’ Alisema Laurent Bujirike raia wa Bukavu.
Wenzake, Musafiri Ashuza pia kutoka Bukavu, na Salomon Kisaka kutoka Beni, pia hawawezi kupokea fedha tangu M23 walipoingia Goma na Bukavu.
‘‘Sasa hivi nikipokea ujumbe nakuwa na wasiwasi. Wanahitaji msaada ila sasa hatujui tutawasaidia namna gani.’’ Walisema wanafunzi hao.

Safari ya Ashuza kurudi nyumbani kuwasalimu wapendwa wake huko Goma, pia imekwama.
‘‘Mbona jamii ya kimataifa haitaki kuwaambia watu wanaotatiza usalama waache kufanya hivyo.’’ Alisema Safari ya Ashuza, mkaazi wa Goma.
Mwanasaikolojia, Daktari Geoffrey Wango, anasema, kuna haja ya walimu kuwaelewa wanafunzi kutoka DRC, wanaopitia hali ngumu kutokana na vita katika nchi yao.
‘‘Wako na msongo wa mawazo kwa sababu wanafikiria mambo ya nyumbani.’’ amesema Mwanasaikolojia, Daktari Geoffrey Wango.
Wanafunzi hao wanasema wamesalia na kushikilia tumaini tu kuwa suluhu la mzozo huo litapatikana.
Douglas Omariba, RFI Nairobi.