Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Belfast wamfukuza Clinton, wasema anatetea mauaji ya kimbari Gaza

Polisi wa Ireland Kaskazini wamemuokoa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton kwa kumuondoa kwenye Chuo Kikuu cha Malkia huko Belfast ambapo mamia ya wanafunzi walikusanyika kulaani msimamo wake kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza.

Mapigano yalizuka katika chuo hicho jana Alhamisi wakati polisi walipoingia ili kukabiliana na wanafunzi waliokuwa wamekusanyika kupinga hotuba ya Hilary Clinton chuoni hapo.

Taasisi ya QUB Palestine Assembly ambayo iliandaa maandamano hayo imesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba wanafunzi wanne wamekamatwa na Huduma ya Polisi ya Ireland Kaskazini.

Kundi hilo pia limesambaza video zinazoonyesha askari polisi wakiwashambulia watu waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Kukamatwa huko kulifanyika wakati mamia ya waandamanaji walipofanya maandamano nje ya Chuo Kikuu cha Malkia, Belfast kupinga hotuba ya Clinton katika Mkutano wa Siku tatu wa Global Innovation na risala uliyokuwa imepangwa kuwasilishwa na mjumbe maalumu wa Marekani huko Ireland Kaskazini, Joe Kennedy.

QUB Palestine Assembly imeshutumu Chuo Kikuu cha Malkia kwa kuwaalika wawili hao ambao imewataja kuwa ni “wahalifu wa kivita.”

Taarifa ya QUB Palestine Assembly imesema: “Clinton amekuwa mtetezi mkubwa wa mauaji ya kimbari yanayofanywa dhidi ya Wapalestina huko Gaza, na Kennedy anawakilisha utawala ambao umesimamia usambazaji wa mabomu na silaha zilizochukua uhai wa maelfu ya Wapalestina.”