Wanafunzi kidato cha tano kupewa kompyuta mpakato, wadau watoa neno

Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023  na mitaala iliyoboreshwa  ukianza kwa baadhi ya madarasa ya shule za msingi na sekondari, bado kuna upungufu wa vitabu vya kujifunzia hali ambayo inaweza kutishia uwezo wa wanafunzi kujifunza kwa ufanisi.

Takwimu zinaonesha uwiano wa vitabu na wanafunzi ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu katika masomo yasiyokuwa ya sayansi,  huku kwenye masomo ya sayansi uwiano ukiwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Kukabiliana na changamoto hiyo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imewaita wadau kushiriki katika kampeni maalumu ya kuchangia ununuzi wa vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, sambamba na kusambaza kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa kidato cha tano.

Kampeni ya ‘Kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja’ inalenga kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja yaani.

Utekelezaji wa kampeni hiyo ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 50 ya  taasisi hiyo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 13 ya mwaka 1975.

Akizungumza leo Februari 20, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Aneth Komba amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha wanafunzi katika maeneo yote wanapata vitabu,  lakini kwa hali ilivyo sasa bado hakuna ulinganifu kwenye uwiano wa vitabu na idadi ya wanafunzi.

Dk Aneth amesema kampeni hiyo inalenga kukusanya fedha zitakazowezesha kuchapwa kwa vitabu 54 milioni sambamba na kusambaza kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa kidato cha tano katika mikoa 10 ya Tanzania.

“Mtalaa wetu ulioboreshwa unasisitiza matumizi ya Tehama, kwahiyo katika fedha zitakazokusanywa kuna kiasi kitatumika kununua kompyuta kwa wanafunzi wa kidato cha tano katika mikoa 10 ya kuanzia.

“Hawa badala ya kupewa vitabu katika nakala ngumu, watapewa laptop ambazo zitakuwa zimewekwa nakala laini za vitabu vya masomo yote. Wizara itaamua mikoa hiyo ni ipi ila itahusisha Tanzania bara na visiwani,”amesema.

Hata hivyo Dk Aneth amesema kabla ya kuhamia kwenye matumizi ya dijitali,  taasisi hiyo imeanza utafiti wa kuangalia namna teknolojia ya akili mnemba inavyoweza kutumika kuanda vitabu na kufundishia.

Amesema: “Tunatambua uwepo wa teknolojia ya akili mnemba lakini tunahitaji matokeo ya utafiti ambayo yatatujulisha tuchukue hatua gani katika ujifunzaji na ufundishaji.

Hata hivyo, wadau wa elimu wameonesha mitazamo tofauti kuhusu hatua hiyo wakiwepo wanaopongeza hatua ya jamii kushiriki kwenye elimu,  huku wengine wakieleza kuwa kutokana na unyeti wa sekta ya elimu Serikali inapaswa kuipa kipaumbele.

Akizungumza na Mwananchi Bahati Abasi ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari amesema kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuchangia kwenye elimu.

“Ni muhimu tukajenga huu utamaduni, kama tunavyochangia sherehe tuone haja ya kuchangia elimu tusiishie kuwa walalamikaji. Kila siku tunasikia kuna uhaba wa vitabu tujiulize tunafanya nini angalau kupunguza uhaba huo kwahiyo naona sawa tuchangie watoto wapate vitabu,”amesema Bahati.

Kwa upande wake mdau wa elimu,  Ochola Wayoga amesema licha ya kampeni hiyo kuwa na nia njema ni vyema ikatafutwa suluhisho la kudumu la kuhakikisha kuna uwiano mzuri wa vitabu na wanafunzi.

“Wadau wanaweza kuchangia vikanunuliwa hivyo vitabu kwa sasa,  lakini nafikiri ni muhimu ukawepo mpango endelevu katika eneo hili la vitabu kwa sababu kila mwaka wanaingia wanafunzi wapya kwenye mfumo wa elimu.

“Katika hilo la matumizi ya teknolojia nalo si baya ila ni lazima tuwe makini kuhakikisha lengo linafikiwa, wenzetu wa Kenya walijaribu hili lakini likashindikana sisemi kwamba kwetu litashindwa ila ni vyema tukajipanga vizuri,” amesema Wayoga.

Kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya TET, Dk Aneth amesema yatatanguliwa matembezi ya hisani ya kilomita 5 yatakayofanyika Machi 7, 2025 yatakayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, yakilenga kukusanya fedha zitakazotumika kwenye uchapaji na usambazaji wa vitabu.