
Dodoma. Wanafunzi 21 wanaosoma kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari ya Mvumi Mission iliyopo wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma wamepelekwa hospitali kupata matibabu wakidhamiwa kula chakula chenye sumu.
Hayo yametokea leo Jumanne Februari 11, 2025 asubuhi baada ya wanafunzi hao kuanza kuharisha na kutapika mfululizo baada ya kula chakula cha usiku.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema, wanafunzi hao walianza kuumwa matumbo baada ya kula chakula cha usiku shuleni hapo na ilipofika asubuhi hali ilikuwa mbaya ambapo walikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi.
Amesema takribani wanafunzi 45 wamekimbizwa kwenye hospitali ya Mvumi Mission kwa ajili ya matibabu zaidi kwa sababu ya kuharisha na kutapika usiku kucha.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mvumi Mission, Dk Albert Chalinze akizungumza na Mwananchi amekiri kuwapokea wanafunzi hao hospitalini hapo na kusema hali zao siyo mbaya ambapo wengine wametibiwa na kuondoka, huku wengine wakibaki kwa ajili ya uangalizi wa afya zao.
Amesema wanafunzi hao walipata mchafuko wa tumbo baada ya kula chakula cha usiku ambacho kilikuwa ni makande.
“Ni kweli nimepokea watoto 21 wanaonekana wamekula food poison, maana walikuwa wanalalamika kuumwa tumbo na kutapika lakini hali zao siyo mbaya, wengine tumeshawatibia wameondoka wamebaki wachache ambao nao hali zao siyo mbaya baada ya muda tutawaruhusu kuondoka,” amesema Dk Chalinze.
Hili ni tukio la pili kutokea mkoani Dodoma ambapo Januari 12, 2025 watoto wanne wa familia moja walikula kitu kinachodhaniwa ni sumu na mmoja wapo alipoteza maisha.
Tukio hilo lilitokea mtaa wa Msangalalee kata ya Dodoma Makulu, mkoani Dodoma ambapo watoto hao walikula kitu kinachodhaniwa kuwa ni mbolea ya chumvi chumvi iliyokuwa imemwagwa korongoni na watu wasiojulikana ambapo mmojawapo alipoteza maisha katika tukio hilo.