Wanafunzi 15 mbaroni wakidaiwa kufanya vurugu Sanya Day

Siha. Wanafunzi 15 wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Sanya Day, Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro wanashikiliwa na polisi mkoani humo kwa tuhuma za kufanya vurugu shuleni hapo na kutaka kuchoma moto nyumba ya mwalimu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka, amethibitisha kukamatwa kwa wanafunzi hao leo Jumatano Novemba 20, 2024 kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17, mwaka huu.

Dk Timbuka amesema vurugu hizo zinatokana na mmoja wa wanafunzi kukutwa na simu na walinzi shuleni hapo na kutoa taarifa kwa mmoja wa walimu, kitendo alichosema hakikuwafurahisha wanafunzi hao.

“Ni kweli tukio limetokea la wanafunzi kufanya vurugu na kutaka kuchoma moto nyumba ya mwalimu, jambo hili si jema na tayari lipo kwenye vyombo vya sheria linashughulikiwa na sisi tunasubiri taratibu nyingine za kisheria kufuata mkondo wake,” amesema Dk Timbuka.

Dk Timbuka amedai siku ya tukio, DC Timbuka amesema: “Baada ya kuona wameshtakiwa kwa mwalimu, walianza kuwarushia mawe walinzi hao, hali iliyozua mtafaruku na baadaye usiku walikusanyika na kutaka kuchoma moto nyumba ya mwalimu, lakini kwa bahati nzuri moto huo uliwahiwa ukazimwa, japo ulikuwa umeunguza eneo dogo la mlangoni,” amesimulia mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu wa wilaya ametoa rai kwa wanafunzi kuzingatia kilichowapeleka shuleni na watambue kwamba wazazi wao wanatumia gharama kubwa kuwaandalia maisha yao bora ya baadaye.

“Kama simu zinakatazwa, mtu anatakiwa kuzingatia, wawapo shuleni wafuate sheria na kuzingatia utaratibu na kanuni zinazowaongoza,” amesisitiza.

Amesema mwanafunzi asipotimiza wajibu wake, ni wazi anamwingizia hasara mzazi wake na hata Serikali wanaotumia gharama kubwa ili kuhakikisha mwanafunzi huyo anafikia ndoto yake.

“Wazazi wanapoteza gharama, Serikali inapoteza gharama ili wao wapate elimu, sasa wasipotimiza hilo, watakuwa hawajajitendea haki wao wenyewe, wazazi wao na Taifa Kwa ujumla,” amesema Dk Timbuka.

Alipotafutwa mkuu wa shule hiyo, Badi Mmbaga kuzungumzia suala hilo, amesema hawezi kulizungumzia na akataka atafutwe mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha.

Hata hivyo, jitihada za kumtafuta Mkurugenzi huyo, Dk Haji Mnasi hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu bila kupokewa.

Diwani wa Kata ya Nasai, Humphrey Kifum ameeleza kusikitishwaa na kitendo hicho na kuwataka wanafunzi kuzingatia masomo badala ya mambo mengine.

“Wasubiri wakihitimu masomo yao wakirudi uraiani watazikuta simu zipo nyingi tu, wakumbuke wanatoka sehemu mbalimbali na katika mazingira tofauti, mtu umefika kidato cha sita unafanya vitu kama hivyo, haipendezi,” amesema diwani huyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi.