
Shinyanga. Wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) mkoani Shinyanga wamesema mzunguko mdogo wa biashara umesababisha washindwe kulipia Sh20, 000 kwa ajili ya vitambulisho vya kidijitali vitakavyowafanya watambulike serikalini.
Hadi Februari 14, 2025 ni wamachinga 178 pekee kati ya 28,111 waliopo mkoani Shinyanga waliolipia fedha hiyo na kukabidhiwa vitambulisho hivyo vitakavyodumu kwa miaka mitatu.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 16, 2025 Mwenyekiti wa wamachinga mkoani humo, Mupinda Mboisa amesema mzunguko wa biashara si mzuri sababu biashara moja inaendeshwa eneo moja na watu wengi, akitolea mfano wauzaji wa urembo na biashara ya chakula.
“Mwitikio wa vitambulisho umekuwa mdogo kati ya 28,000 ni 178 tu waliokamilisha na kupewa, changamoto kubwa ni mzunguko wa biashara,” amesema Mboisa.
Mmoja wao mwenye kibanda cha kuuza jezi katika soko la Ibinzamata, Juma Bakari ameeleza kuwa hata mwingiliano mdogo wa watu kwenye soko hilo unachangia hali ngumu ya biashara, hivyo kushindwa kugawa fedha kwa ajili ya kitambulisho hicho.
“Changamoto iliyopo katika biashara zetu katika soko hili hakuna mwingiliano wa watu, wateja wengi huja kununua mahitaji ya kupikia unaweza kumaliza hadi siku tatu hujauza na nyumbani wanakutegemea, kutoa 20,000 ni changamoto” amesema Bakari.
Mamalishe anayeuza mihogo Shule ya Msingi Mwenge, Monica Matonange amesema, “biashara yangu kwa asilimia kubwa inategemea wanafunzi ambao nawauzia kwa Sh100, kuzikusanya hadi kufika 20,000 ni mauzo ya biashara yote, bado sijatoa matumizi, faida yenyewe hata nusu ya mauzo haifiki, alisema.”
Hata hivyo, Hildefonce Kamugisha amesema mpango wa Serikali kuwatambua wafanyabiashara wadogowadogo ni muhimu kwa kuwa umerahisisha kupata mikopo kwenye benki pamoja na kutambulika.
“Hii imerahisisha njia ya kupata mikopo wa sababu hapo awali tulikuwa tunaambiwa tuwe na mali isiyohamishika, ndio unapata mkopo lakini kupitia kitambulisho hiki cha kidijitali taarifa zetu zitasomeka katika taasisi zote za Serikali na kibenki” amesema Kamugisha.
Jana wakati akizindua na kugawa vitambulisho hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema Serikali inahitaji kuwatambua ili iwaandalie mazingira mazuri ya kufanya biashara, na utambuzi huo ni wao kuwa na vitambulisho hivyo.
“Serikali inahitaji kuwatambua wafanyabiashara wadogowadogo ambao mtaji wao unaanzia Sh1 hadi Sh4 milioni, ambao taarifa zao zitakuwa zinafahamika ili kuwajengea mazingira ya kukua kibiashara na upatikanaji wa fursa na mikopo” amesema Macha.
Kaimu Katibu Tawala mkoani humo, Samson Hango amesema vitambulisho hivyo havitoi msamaha kwa kodi wala tozo mbalimbali zitakazotozwa na Serikali.
“Tozo zitakazotozwa na serikali za mitaa au serikali kuu zinatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo vitambulisho hivi, havimzuii mfanyabiashara kulipa tozo na kodi zilizowekwa” amesema Hango.
Pia Hango amesema kuwa Mkoa wa Shinyanga una wafanyabiashara wadogo 28,111 lakini hadi sasa umepokea vitambulisho 178 vya waliokamilisha utaratibu.
Ili mfanyabiashara aweze kupata mkopo lazima awe na miaka 18 na kuendelea, amejiandikisha na kupata kitambulisho cha Machinga na eneo maalumu la kazi (anwani).