Walipakodi wataka kundi dogo, la kati kutambuliwa na TRA

Dodoma. Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma ikivuka lengo kwa kukusanya Sh98.2 bilioni kwa kipindi cha miezi sita, walipakodi wameshauri kutambuliwa kwa kundi la kati na dogo ili kuongeza wigo wa walipakodi.

Oktoba 4, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, alisema ni watu milioni mbili tu ndiyo wanalipa kodi kati ya watu milioni 37 ambao walipaswa kukatwa kodi.

Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Pendolake Elinisafi ameyasema hayo leo Ijumaa, Februari 14, 2025 baada ya matembezi ya maadhimisho ya siku ya mlipakodi.

Elinisafi amesema kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2024, walikuwa na lengo la kukusanya Sh98.2 bilioni lakini walikusanya Sh101 bilioni ambayo ni ufanisi wa asilimia 103.

“Mwenendo wetu wa kukusanya kodi unaenda vizuri na tunategemea hadi kufika Juni, 2025 tutakuwa tumevuka lengo ambalo tunalengo la kukusanya Sh190 bilioni kwa mwaka,” amesema.

Elinasafi amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano ambao wanapata kutoka kwa walipakodi ambapo kwa sasa kuna masikilizano na ushirikiano.

Amesema kila siku ya Alhamisi ni siku ya kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao huku akiwahamasisha Watanzania kuacha kukwepa kulipa kodi.

Naye Mgeni rasmi katika matembezi hayo, Mchumi wa Mkoa wa Dodoma, Francis Kaunda amewaasa Watanzania kutumia siku ya mlipa kodi kwa kulipa kodi kwa hiari na wasisubiri kulazimishwa.

“Endeleeni kutoa elimu kwa walipakodi ili wafahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati. Tunaona Serikali ya awamu sita imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa wakati. Miradi yenye kujikita kuhakikisha huduma za afya, elimu na maji na nyingine zinatolewa,” amesema.

Ametoa wito kwa TRA kutoa ushirikiano na elimu ya mlipa kodi mara kwa mara ili Watanzania wajue na wawe na nia njema ya kulipa kodi bila kuwa na bughudha yoyote.

Mmoja wa walipakodi nchini na mfanyabiashara jijini Dodoma, Peter Olomi amesema maadhimisho hayo ni jambo jema kuendelea kuwatambua walipakodi ambao hawajulikani mitaji yao ilitoka wapi.

“Licha ya kutojulikana walipotoa wanajitoa kwa ajili ya kushirikiana na Serikali kusababisha maendeleo na kuunga mkono kukuza maendeleo ya kiuchumi ya nchi,” amesema.

Amesema ni vyema siku hiyo ikatumika katika kuongeza makundi tofati kwa sababu kundi la walipakodi wakubwa huwa ndilo linatambuliwa kwa kupewa vyeti wakati wa maadhimisho hayo.

“Liangaliwe kundi la kati na dogo, lile kundi la kati na dogo likitambuliwa ambapo ndio kuna wengi litahamasika, hawatachukulia kuwa kodi ni maumivu, uonevu ama chochote kibaya bali ni jambo zuri, watachukulia Serikali inajali,” amesema.

Amesema eneo ndilo linatakiwa sana kujenga urafiki kati ya mtoza kodi na mlipakodi hasa wakionyesha kazi zilizofanyika kwa kutumia kodi zao wanazozitoa.

Olomi amesema zikiainishwa kazi zinazofanyika na kuwaambia kuwa wanatambua wao ni watu muhimu, ana uhakika kuwa hakutakuwa na pengo linalowafanya wafanyabiashara wa kati na wadogo kukimbiana kama inavyoonekana hivi sasa mtaani la watu kufunga maduka.