
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu Watanzania 36 kulipa faini ya Sh30,000 kila mmoja au kwenda jela miezi mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuondoka nchini Tanzania na kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.
Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Said Bura (25) mkazi wa Kizuia, Allen William (21) mkazi wa Mwanza, Hamad Magimaba (25) mkazi wa Charambe, Baton Tarimo (31) mkazi wa Kinondoni, Jovin Nguma (45) mkazi wa Sinza, Joseph Mkunde (37) mkazi wa Kigogo na wenzao 30.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Machi 12, 2025 Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Geofrey Mhini, baada ya washtakiwa kukiri kosa lao na mahakama kuwatia hatiani kwa kosa hilo.
Hakimu Mhini alisema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa na wamekiri wenyewe shitaka lao, hivyo anawahukumu kila mshtakiwa kulipa faini Sh30,000 na wakishindwa watakwenda jela miezi mitatu.
Akiwasomea maelezo ya awali, Wakili kutoka Uhamiaji, Raphael Mpuya akishirikiana na Hadija Masoud alidai washtakiwa waliondoka nchini bila kufuata taratibu wa uhamiaji wa kutoka na kuingia nchini.
Alidai washtakiwa hao walikwenda Afrika Kusini wakitegemea watapata maisha mazuri na badala yake walikuwa wanazurura kwa sababu walikuwa hawana kazi Afrika Kusini, hivyo walikamatwa na kupelekwa gerezani.
Mpuya alidai washtakiwa waliondoka nchini kwa kutumia usafiri wa barabara na walikuwa wanapita mipaka isiyojulikana na waliondoka bila kuwa na hati ya kusafiria.
“Watuhumiwa walipita bila kukaguliwa na maofisa wa uhamiaji na hivyo kufanya uondokaji wao nchini kuwa kinyume cha sheria,” amedai Mpuya na kuongeza.
“Baada ya kutoka walipita nchi tofauti mpaka walipofika nchini Afrika Kusini ambapo waliingia bila kufuata sheria na washtakiwa hawa waliendelea kuishi nchini humo mpaka walipokamatwa katika misako na doria kwa nyakati tofauti na walishikiliwa magereza tofauti nchini Afrika Kusini,” amesema wakili Mpuya.
Hata hivyo, Machi 5, 2025 washtakiwa walirudishwa nchini Tanzania kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Baada ya kuwasili JNIA walikamatwa na maofisa wa uhamiaji kwa tuhuma za kuondoka nchini Tanzania kinyume cha sheria.
“Baada ya kukamatwa washtakiwa walipelekwa ofisi ya Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na taratibu nyingine zilipokamilika, leo wamefikishwa mahakamani,” alisema Mpuya.
Baada ya kuwasomea maelezo yao, washtakiwa wote walikiri shitaka lao linalowakabili na ndipo walipotia hatiani kama walivyoshtakiwa.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao Godfrey Mpandikizi kutoka Taasisi ya Tanzania Anti-Human Trafficking and Legal Initiatives (TATLI) aliomba washtakiwa wapewe adhabu ndogo kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza.
Kwa upande wa mashitaka waliomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe funzo kwa wengine.
“Washtakiwa hawa wamekuwa wakiitia Serikali hasara kwa kuwasafirisha washtakiwa hawa kutoka Afrika Kusini hadi hapa nchini kwa kutumia ndege ya Serikali, hivyo wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria,” alisema Mpuya.
Hakimu Mhini baada kusikiliza shufaa za pande zote mbili, aliwahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh30,000 kila mmoja au kwenda jela miezi mitatu iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Machi 5, 2025 JNIA uliopo Wilaya ya Ilala, wakiwa raia wa Tanzania, waliondoka isivyo halali katika ardhi ya Tanzania bila kibali na kuelekea Afrika Kusini.