
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imewahukumu adhabu ya kifo, watu wawili waliovamia Benki mbili za CRDB na Benki ya Biashara ya DCB za jijini Dar es Salaam na kuua watu watatu kwa mtutu wa bunduki.
Tukio hilo la mauaji lilitokea saa 8:40 mchana wa Desemba 8, 2015 katika eneo la Chanika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa uvamizi wa benki hizo ambapo miongoni mwa waliouawa ni walinzi wawili wa Suma-JKT.
Waliouawa wametajwa kuwa ni Ramadhan Rashid Halili na Shani Rajabu Mohamed waliokuwa walinzi wa Suma JKT katika Benki ya CRDB na mtu mwingine ambaye ametajwa kuwa ni Gabriel John Ngwangai.
Ingawa hukumu inawataja waliohukumiwa ni washitakiwa ambao ni Mohamed Hassan na Rajabu Ally, lakini Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, kupitia ukurasa wake wa X (Twitter) amewatambulisha watu hao kuwa masheikh.
Hukumu hiyo imetolewa Aprili 28, 2025 na Jaji Butamo Phillip na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa katika tovuti ya Mahakama leo Aprili 30, 2025 ambapo Jaji alimwachia huru mshitakiwa wa tatu, Kulwa Athman kwa kukosekana ushahidi.
Usikilizwaji wa kesi hiyo uliendeshwa pasipo kutaja majina ya washitakiwa wala anuani za makazi ambapo mashahidi wa upande wa Jamhuri walitambulishwa mahakamani kwa namba P25,P43,P22,P7,P27,P20, P23 na namba P24.
Mbali na kutotajwa majina na anuani za makazi yao, lakini mashahidi hao walitoa ushahidi wao wakiwa wamefichwa katika kizimba maalumu kilichowekwa mahakamani ili kutoonekana ili kutotoa utambulisho wao halisi wa sura.
Ushahidi ulivyokuwa
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, alieleza kuwa mwaka 2016 alikuwa miongoni mwa maofisa waliokuwa katika kikosi kazi kilichoundwa kwa ajili ya kufanya upelelezi wa matukio ya ugaidi, ambayo yalihusisha uvamizi wa benki hizo mbili.
Kulingana na shahidi huyo, marehemu katika shauri hilo waliuawa wakati wa uvamizi wa benki hizo ambazo zinatizamana, ushahidi ambao uliungwa mkono na shahidi wa pili wa Jamhuri ambaye alikuwa Ofisa Mfawidhi wa Benki ya CRDB.
Shahidi huyo alieleza kuwa benki hiyo ilikuwa na walinzi wawili wa Suma JKT, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume ambapo mlinzi mwanamke alipangiwa ndani ya benki na mwanamme alipangiwa nje akiwa na bunduki.
Alieleza kuwa Desemba 8, 2015 saa 7:40 mchana, benki yao ilivamiwa na watu wenye silaha ambapo wakati huo alikuwa anapata chakula cha mchana karibu na ofisi yake, na wakati anasubiri aletewe chakula, alisikia milio ya risasi.
Milio hiyo ilikuwa inatokea uelekeo wa benki yake ambapo alikimbilia Kituo cha Polisi Chanika kutoa taarifa na alimkuta Ofisa wa Polisi ambaye alimfahamisha kuwa na yeye amesikia milio hiyo na ametoa taarifa kituo cha Stakishari.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, waliongozana na Ofisa huyo wa Polisi hadi benki na alipofika alikuta wafanyakazi wenzake wakiwa nje wanalia na waliwaeleza kuwa walinzi wote wawili wameuawa na akamuona Ramadhan akiwa amelala sakafuni.
Alikuwa amekufa na alikuwa na matone ya damu chini ya kifua na baadae akamuona mlinzi mwingine, Shani akiwa na majeraha kichwani akiwa naye amelala sakafuni lakini naye alikuwa tayari ameshapoteza maisha.
Shahidi wa nne ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Chanika, alieleza kuwa Desemba 8,2015 alisikia mlio usio wa kawaida wakati huo akitembea umbali wa kama meta 100 kutoka mahali zilipo benki za CRDB na DCB zinazotazamana.
Aliamua kusimama na kutizama ni nini kilikuwa kinatokea ambapo katika kipindi kifupi, alisikia milio ya risasi na akaona watu wakiwa wanakimbia na pembeni ya barabara alimuona mtu akiwa ameshika bunduki anazuia magari yasipite.
Mtu huyo alionekana akiyafatulia risasi magari yaliyolazimisha kupita ili kuwatisha madereva na wakati huo yeye alikuwa umbali wa meta 12 tu kutoka mahali alipokuwa amesimama na akishuhudia purukushani hizo.
Ni wakati huo alisikia majibizano ya risasi kati ya walinzi wa benki hizo mbili na watu hao waliokuwa na silaha, ambapo aliona gari ikija kutokea benki ambapo mtu huyo mwenye silaha alipanda na wakatokomea kusikojulikana.
Shahidi wa sita alieleza kuwa mmoja wa walinzi aliyeuawa, Ramadhan Halili alikuwa mpwa wake ambapo usiku huo huo alipigiwa simu na uongozi wa Suma JKT na alikwenda siku iliyofuata na kujulishwa rasmi kuuawa kwa mpwa wake.
Kwa upande wake, shahidi wa 8 ambaye ni afisa wa polisi aliyekuwa akifanya kazi kituo cha Stakishari katika idara ya upelelezi, ambapo alishiriki katika shughuli ya uchunguzi wa miili ya walinzi hao uliofanywa na daktari ili kubaini chanzo cha kifo.
Baadae alikwenda kumuona Gabriel Ngwangai ambaye alikuwa amelazwa hospitali akiwa na majeraha ya risasi na kusema hata hivyo baadaye naye alifariki kutokana na majeraha mabaya ya risasi aliyoyapata.
Katika utetezi wao, washitakiwa wote hawakuwa na ubishi kuwa marehemu wote watatu hawakufa kifo cha kawaida lakini walidai kuwa kamwe hawakushiriki kwa namna yoyote ile na tukio hilo la CRDB ba DCB na walikuwa hawafahamu lolote.
Hukumu ya Jaji
Akichambua ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Phillip alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa marehemu waliotajwa, waliuawa kwa kupigwa risasi katika uvamizi wa CRDB na DCB.
“Nimeuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi. Hata hivyo hata ushahidi huo haujaleta mashaka yoyote kuwa marehemu waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa uvamizi wa benki hizi mbili hivyo hawakufa kifo cha kawaida,”alisema Jaji.
Katika kuthibitisha kuwa ni washitakiwa ndio waliohusika, Jaji alirejea ushahidi wa shahidi wa kwanza aliyetoa ushahidi kuwa Juni 13,2015 akiwa kituo cha Polisi Tazara, alipata taarifa fiche kuwa mmoja wa walioshiriki ni Mohamed Hassan.
Kwamba alikuwa anaishi Mbagala Misheni karibu na kiwanda cha KTM ambapo mtoa taarifa huyo alimpa muonekano wake na baada ya kupata taarifa hizo walikwenda eneo hilo akiwa na askari wengine nane na kumkamata.
Kulingana na shahidi huyo, katika mahojiano mshitakiwa huyo alikiri kushiriki tukio la uvamizi wa benki hizo ambapo alikubali kutoa ushirikiano na kuwapeleka mahali walipo washirika wake ambao dhamira yao ni kuanzisha Dola la Kiislamu nchini.
Jaji alisema pamoja na ushahidi wa mashahidi wengine, lakini shahidi wa tano ndiye aliandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa huyo wa kwanza na kueleza namna mshitakiwa alivyoshiriki mwanzo mwisho katika tukio hilo.
Shahidi wa saba alieleza namna alivyoandika maelezo ya mshitakiwa wa pili, Rajabu Ally ambapo alifunguka kila kitu na kueleza kuwa baada ya kuvamia benki hizo na kuwaua walinzi hao wawili, walifanikiwa kuiba pia fedha.
Baadae alipewa mgawo wa Sh2.5 milioni ambapo shahidi wa 8 yeye alieleza alivyoandika maelezo ya mshitakiwa wa tatu ambaye ameachiwa na mahakama, ambaye alidai alimweleza kuna watu wanataka kuanzisha Dola ya Kiislamu.
Katika maswali ya Dodoso kutoka kwa wakili wa mshitakiwa huyo, shahidi huyo alidai kuwa kamera za usalama (CCTV) hazikuweza kunasa tukio hilo lakini wahalifu hao waliweza kuiba Sh25 milioni za CRDB na Sh20 milioni za DCB.
Jaji alisema kielelezo namba P2 na P3, vinaonyesha kuwa mshitakiwa wa kwanza na wa pili walieleza ushiriki wao katika uvamizi wa benki hizo mbili, maelezo yanayoshabihiana na taarifa fiche alizokuwa amepewa shahidi wa kwanza.
Vielelezo hivyo ambavyo ni maelezo ya washitakiwa hao, walieleza kwa kirefu juu ya uvamizi huo na kwamba lengo lao lilikuwa kutafuta fedha katika benki hizo ili kuzitumia kununua silaha kutimiza lengo lao la kuanzisha Dola la Kiislamu nchini.
Kwa kuchambua ushahidi huo na vielelezo hivyo, Jaji alisema ameridhika kuwa upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa wa kwanza, Mohamed na wa Pili, Rajabu lakini ulishindwa kwa mshitakiwa wa tatu.
Jaji alisema washitakiwa hao walikuwa na nia ovu kutokana na silaha walizozitumia kwani marehemu walikuwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili hivyo hao wanahukumiwa kifo lakini mshitakiwa wa tatu anaachiwa huru.