
Dar es Salaam. Jumla ya Sh306 milioni zinatarajiwa kulipwa na Shirika la Masoko Kariakoo kwa madeni ya waliokuwa watumishi wa Soko la Kariakoo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 18, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Hawa Ghasia wakati wa kikao cha Kumi cha Bodi hiyo kilichoketi jijini Dar es Salaam.
“Serikali imesikia kilio cha waliokuwa wafanyakazi wa Shirika letu na kutupatia shilingi milioni 306 kulipa madeni.
“Hivyo nataka kuona ifikapo mwisho mwa wiki hii fedha hizo ziwe zimelipwa kwa walengwa kwani wamesubiri kipindi kirefu” ameagiza Ghasia.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Ashraph Yusuph Abdulkarim, amekiri kupokea fedha hizo toka Hazina ikiwa ni kufuatia maombi ya siku nyingi.
“Tunaahidi fedha hizo zitalipwa kwa wastaafu wote waliokuwa wakifanya kazi kwenye shirika letu na kwa kuzingatia umakini ili haki itendeke,” amesema Abdulkarim.
Akitoa takwimu za wanaostahili kulipwa, Meneja wa Fedha wa Shirika, Semeni Yamawe amesema wastaafu 19 watalipwa fedha hizo wakiwemo warithi ambao ndugu zao walikuwa watumishi pamoja na wastaafu ambao walishinda kesi mahakamani.
Katika hatua nyingine, bodi ya wakurugenzi imeelekeza menejimenti ya shirika kusimamia kikamilifu mpango kazi wa kuelekea ufunguzi wa soko la Kariakoo ikiwemo kuwapanga wafanyabiashara kwenye maeneo na kutoa mikataba ili shughuli zirejee sokoni.
Soko la Kariakoo linatarajia kurejesha shughuli zake hivi karibuni baada ya kukamilika kwa ujenzi wake ulioanza angu mwaka 2021.
Soko hilo baada ya kuungua serikali ilitoa Sh28.03 kwa ajili ya kulikarabati ujenzi ulioenda sambamba na kujengwa kwa soko jipya dogo lenye ghorofa nane.