
Hatima ya mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kuendelea kuliwakilisha jimbo hilo iko mikononi mwa wananchi kutokana na vita kali katika jimbo hilo.
Miongoni mwa yanayochochea moto jimboni kwake ni hali ya kuonekana mwanasiasa huyo kukubalika zaidi kwa wananchi, lakini hakubaliki kwa viongozi wengine wa chama katika mkoa huo.
Mpina amekuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2005 na mwishoni mwa Juni 2025, anamaliza muhula wake wa nne kabla ya kwenda kwenye uchaguzi endapo atapitishwa na chama chake kugombea ubunge kwa mara nyingine.
Jimboni kwa Mpina kunawaka moto baada ya kukosekana kwa maelewano mazuri kati yake na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya na mkoa, jambo ambalo linamweka kwenye nafasi ngumu kurejea tena bungeni kama mwakilishi wa jimbo hilo.
Hoja zinazojengwa na wanaompinga zinaeleza kwamba Mpina amekuwa akijitanguliza mwenyewe kwenye miradi ya maendeleo iliyotekelezwa jimboni kwake, badala ya kumtanguliza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye anatoa fedha hizo. Wajumbe hao wanamtuhumu mbunge huyo kama msaliti, mwenye ghiliba ya kujawa na kiburi na anakikosea heshima chama hicho.
Mpina amekuwa mwiba mchungu kwa mawaziri anapokuwa bungeni ambapo amekuwa akiwakosoa waziwazi, akidai wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mawaziri walioonja joto la Mpina ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe. Pia, amekuwa akiwashughulisha mawaziri bungeni kujibu hoja anazokuwa amezitoa kwenye wizara zao.
Wakati viongozi wa Mkoa wa Simiyu na kamati ya siasa ya mkoa huo wakimpiga vijembe Mpina kwenye kikao cha Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, aliyefanya ziara katika Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, mwenyewe amelalamikia kampeni za mapema jimboni kwake.
Hata hivyo, wananchi jimboni kwake wanamkingia kifua kwa kile wanachodai kwamba licha ya maringo na haiba yake ya kutaka kuonekana, kwao Mpina anawafaa, kwa kuwa ni mchapakazi na anafanya maendeleo yanayoonekana na anapaswa kuwa mfano kwa wawakilishi wengine.
Kihongosi arusha vijembe
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi anasema siasa za mkoa huo ni nyepesi kuliko zinavyoonekana na zinavyotamkwa na kupambwa huko nje. Amemhakikishia Wasira kwamba chama hakitapoteza jimbo wala kata.
Kihongosi aliwataka makada wa chama hicho kuishi katika misingi ya uongozi kwa kuzingatia kanuni na katiba ya chama hicho ili kikapate ushindi wa kishindo 2025.
“Tunaenda kushinda, aletwe Juma, Mwanaisha au Hussein atashinda, chama hiki hakina mtu maarufu, wote mnaoona wana umaarufu wameupata kwa sababu ya CCM, lakini ikikuvua uCCM wako, wewe ni mtu wa kawaida,” anasema.
Kihongosi, ambaye pia ni kamisaa wa chama hicho, anasema anaheshimika kama Mkuu wa Mkoa kwa sababu mwenyekiti wa chama hicho amemteua kushika wadhifa huo, lakini akitenguliwa ni mtu wa kawaida, heshima yake ni kwa sababu ya chama hicho.
“Wabunge hawa wanaheshima hizi kwa sababu ya chama, lakini chama kikichukua uanachama wake, hatakuwa na heshima yoyote, atakuwa mtu wa kawaida. Kwa hiyo, asisimame mtu yeyote mahali popote ndani ya mkoa huu akaamini ana nguvu kuliko chama, atakuwa anajidanganya,” anasema.
Mwenyekiti mkoa aonya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed anasema mkoa huo uko salama, ingawa watu wanasema unaweza kuona bodi limechoka, lakini injini iko safi na inafanya kazi kwa ufanisi.
“Mkoa wa Simiyu unaongozwa na vijana na hatutetereshwi na vijana, napenda nilizungumzie hili, Meatu kumekuwa na maneno mengi ambayo yanatumika kutengenezeana ajali, hata juzi nimesikia.
“Tuache kutengenezeana ajali, chama hiki kina utaratibu, kinateua wanaoweza kugombea 20, lakini Mungu akambariki mmoja, akaja kushinda, sasa hivi tuna vurugu za kwenda kwenye uchaguzi ndiyo maana watu wako matumbo joto,” anasema na kuongeza:
“Kila alichopanda mtu, ataenda kukivuna. Kwa hiyo tusitengenezeane ajali, kama ulipanda mema kwa wananchi utavuna mazuri kwa wananchi na kama hukufanya hivyo, huwezi kuvuna. Chama hiki kina utaratibu, ukifika muda kila mtu anaruhusiwa kugombea, hakuna mwenye haki miliki ya kata wala jimbo,” anasema.
Anasema pamoja na maneno mengi ya kuchongeana kwenda juu, lakini Wilaya ya Meatu yenye majimbo mawili ya Meatu na Kisesa, watafanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. “Nikuambie Makamu Mwenyekiti, kuna watu wengine wanatishia kukihama chama wakija tutakuletea kwako kwamba wametoka CCM, ninaomba tuwaruhusu waendelee lakini chama kitaendelea na ushindi ni lazima kwa CCM,” anasema.
Alia kampeni za mapema
Akizungumza kwenye mkutano huo huku akishangiliwa na makada wa chama hicho kwenye mkutano huo, mbunge wa Kisesa, Mpina anasema katika jimbo lake wamejitokeza makada wengi wanapiga kampeni, wanadai ni watia nia.
“Watia nia, watia nia, lakini chama hakiruhusu watu kujitokeza mapema na kuanza kufanya kampeni na walikuwa wanafanya kampeni usiku, nikasema hizo kampeni zenu na utia nia wenu fanyeni mchana na usiku ili mpate fursa nzuri zaidi, nilishazoea mapambano,” anasema Mpina.
Anasema amekuwa mbunge kwa miaka 20, na mjumbe wa kamati ya siasa kwa miaka 22 na amekuwa mwalimu na wanafunzi wake wanaojipitisha waruhusiwe kufanya kampeni usiku na mchana.
“Waruhusuni wafanye kampeni usiku na mchana halafu wasuburi ili wasije wakapata kigezo kingine chochote. Ninachotaka kusema ni wajumbe wangu wa halmashauri kuu kazi nzuri iliyofanywa na CCM, tunachohitaji ni mshikamano pale tutakapokuwa tumempata kada sahihi kwenye maeneo yote mawili, udiwani na ubunge, basi umoja wetu usivunjike,” anasema.
Mpina anasema amedhamiria na kuapa hakuna kupumzika hadi maendeleo yapatikane. Amesisitiza kwamba “siwezi kutishwa na chochote”.
Busara za Wasira
Akizungumza kwenye mkutano huo, Wasira alisema Wilaya ya Meatu inaongoza kwa kuwa na makundi na taarifa mbaya ni nyingi, huku akidai anashindwa kuelewa kwa nini wanashindwa kutazama sifa hizo zinazosambaa.
“Hatutakubali kuuacha mtumbwi uendeshwe na vijana, unaweza kutoboka bila kufika tunakokwenda, Meatu mmezidi. Chanzo cha mgogoro na kuibuka makundi haya ni fedha, mtu akishindwa anataka asishindwe, anabaki na kundi lake.
“Hawa watu wangu unasema wako wakati ni watu wa Mungu, hata CCM tunatumia watu wa Mungu, wewe wa kwako uliwatoa wapi?” anahoji.
Anasema watu wanatumia fedha nyingi, mwisho wa siku yanaibuka makundi na kutengeneza chuki kubwa kwa muda wote wa miaka mitano.
Wananchi wamkingia kifua
Judith Fabian, mkazi wa Meatu mkoani Simiyu, anasema mvutano uliopo baina ya pande hizo ni mkubwa, ingawa Mpina anakubalika zaidi kwa wananchi baada ya kuwafanyia mazuri.
“Binafsi sioni ubaya kujisifia kama miradi inatekelezwa katika jimbo lake, sasa hawa wanataka kila wakati aseme Rais amefanya, kwani akijisifia si inajulikana fedha zinazotumika kutekeleza miradi ni kodi zetu,” anasema.
Ameongeza kuwa Mpina ni kiongozi mzuri pamoja na udhaifu wake wa kutaka kujiona, lakini mengi anayoyafanya yanaonekana jimboni kwake tofauti na wengine.
Kwa upande wake, Rose Nyatunzi anasema Mpina anakubalika, lakini anaogombana nao ni kama wameshika makali, wanaweza kumuondoa mchezoni, hawataki aendelee kugombea nafasi hiyo.
“Amekuwa na mvutano na baadhi ya viongozi wa kiserikali, lakini ukiangalia hoja anazosimania zina mashiko, sasa anaonekana mbaya,” anasema.