
Dar es Salaam. Waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) walioondolewa kazini kutokana na kuwa na vyeti vya darasa la saba, wamemlilia Rais Samia Suluhu Hassan wakimuomba awasaidie ili walipwe stahiki zao.
Wamesema stahiki hizo ni haki ya malipo ya kujikimu wakati wakisubiri kurudishwa maskani kwao katika kipindi cha miaka minne, pamoja na haki ya malipo ya utumishi kwa kipindi chote cha utumishi wao.
Wamedai kusotea malipo yao TPA huku wengine wakilalamika kulipwa fedha pungufu ambazo haziendani na uhalisia wa kile walichostahili kupata baada ya kuondoshwa kazini mwaka 2018.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai ya wafanyakazi hao, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema tayari wamelipwa na hakuna wanachokidai.
Wafanyakazi hao wa zamani walidai kuwa walistahili kulipwa Sh157,000 kwa siku katika kipindi cha miaka minne, lakini malipo waliyopokea ni Sh800,000 na wengine hadi Sh5 milioni ambayo ni pungufu ya walichostahili.
Wakizungumza na Mwananchi leo Machi 26, 2025, wafanyakazi hao wa zamani wamedai malipo hayo ni haki yao kwa kuwa waliajiriwa na kufanya kazi TPA kwa sifa za vyeti vya darasa la saba na siyo vyeti feki.
“Sisi hatukupata ajira bila sifa, tuliajiriwa kwa elimu yetu ya darasa la saba, hatukudanganya, iweje leo tusilipwe stahiki zetu,” alihoji mwenyekiti wa kamati ya wafanyakazi hao, Mathias Mazengo ambaye alifanya kazi TPA tangu mwaka 1997 kama dereva wa kutoa magari kwenye meli na kuyaegesha yadi.
Hamis Mzenga, aliyekuwa askari wa bandari, amedai katika kipindi cha miaka 10 kazini, alicholipwa kama stahiki yake ni Sh3,200 ya nauli yeye na familia yake na mshahara wa mwezi mmoja sambamba na Sh238,000 ya gharama za mizigo.
“Hivi kweli kwa miaka 10 niliyokuwa kazini, nalipwa Sh3,200 ya nauli mimi na familia yangu? Basi nifanyiwe hivi nikiwa kweli nimefoji, lakini niliajiriwa kwa sifa ya cheti cha darasa la saba,” amesema Mzenga huku akiungana na wenzake kumuomba Rais Samia kuwasaidia kuagiza uchunguzi wa uhalali wa malipo hayo ili haki itendeke.
Akilifafanua hilo Mbossa amesema, “wamelipwa kulingana na taratibu, kila kitu kililipwa, labda kama kuna utaratibu mpya, lakini walichotakiwa kulipwa walilipwa,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu madai ya wafanyakazi hao ya kutakiwa kulipwa Sh157,000 kwa siku katika kipindi cha miaka minne kila mmoja, Mbossa alihoji malipo hayo wanayataka pamoja na kufoji vyeti.
“Utaratibu uliotolewa wa malipo ya waliokuwa na cheti cha darasa la saba na wenye vyeti vya form four (kidato cha nne) ulitolewa na nani?” amehoji Mbossa na kuongeza:
“Hakuna ambacho hawajalipwa, walichostahili kulipwa kutokana na utaratibu uliotumika, kama kuna chochote ambacho hawajalipwa wanajua pa kwenda,” amesema.
Magumu wanayopitia
Otilia Faida, aliyekuwa muhudumu wa ofisi, amezungumza huku akilia akisema wanaishi katika kipindi kigumu cha maumivu na mateso.
“Nilishindwa kuwasomesha watoto, kinachoniumiza zaidi sikufoji cheti, nilikuwa mfanya usafi TPA tangu mwaka 2008 hadi 2010, nikaajiriwa,” amesema kwa masikitiko.
“Naumia kuona natesekea stahiki yangu, tunafahamu kurudi kazini sio rahisi, maana sisi tulioishia la saba hatuna kitu, wanilipe stahiki zangu, tunamuomba Rais Samia atusaidie katika hili,” amesema.
Happy Mwaitenda, aliyekuwa askari wa TPA tangu mwaka 2007, amesema msaada pekee kwao ni Rais Samia kulifuatilia suala lao.
“Mimi nililipwa Sh800,000 katika kipindi chote kazini, stahiki yangu ni Sh800,000,” amehoji Mwaitenda huku akibubujikwa na machozi.