Waliomuua, kukata uke wahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Geita. Methali ya kusema “ukiua kwa upanga, utakufa kwa upanga” inaonekana kutimia baada ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, kuwatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa watatu waliohusika katika mauaji ya Joyce Lundeheka (51).

Washtakiwa hao walikutwa na hatia ya kumuua Joyce kwa kumkata na kitu chenye ncha kali, kisha kukata sehemu za siri (uke) na kuondoka nazo na kwenda kuzitakasa kwa mganga wa kienyeji.

Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa wanne, ambapo watatu kati yao ni dada wa marehemu, Thereza Luhedeka (73), Mateso Joseph (23), mtoto wa Thereza; na Elias Galawa (49), mganga wa kienyeji walihukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Hata hivyo, Dogan Budeba aliachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa lake.

Akitoa hukumu hiyo Machi 28, 2025, Hakimu Mkuu, Fredrick Lukuna alieleza kuwa Mahakama hiyo imezingatia kwa makini ushahidi wa upande wa mashitaka kabla ya kufikia uamuzi huo.

Hakimu Lukuna aliweka wazi kwamba ushahidi uliotolewa, ikiwa ni pamoja na mashahidi 16, ulikuwa thabiti na kuthibitisha bila shaka kwamba washtakiwa walihusika katika tukio hilo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa walijitetea binafsi, wakiwa na msaada wa jopo la mawakili wanne.

Wakili Bathlomeo Msiyang alimtetea mshtakiwa wa kwanza, Doreen alimtetea mshtakiwa wa pili, Angel Mbaga alimtetea mshtakiwa wa tatu, na Wakili John Paul alimtetea mshtakiwa wa nne.

Hakimu Lukuna, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, alisema kwamba kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha pasipo shaka yoyote kwamba washtakiwa wote watatu walihusika katika mauaji ya Joyce Ludeheka.

Aliongeza kuwa hukumu hiyo imetolewa kama fundisho kwa wengine ili kuepuka vitendo vya aina hiyo.

Kesi hiyo ya mwaka 2024, ilianza kusikilizwa Januari 2025, ambapo upande wa mashitaka uliongozwa na Wakili wa Serikali, Liberatus Rwabuhanga, akisaidiana na mawakili Ipyana Mwantonto na Scholastica Tiffe.

Washtakiwa hao walimuua Joyce Ludeheka Oktoba 11, 2023, akiwa nyumbani kwake, kwa kumkata na kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake. Vitendo vyao vinakiuka kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo, baada ya kumuua Joyce Ludeheka, washtakiwa walikata sehemu za siri za marehemu na kutoweka nazo.

Walikamatwa baadaye, ambapo ilibainika kuwa walizikausha sehemu hizo kwa mganga wa kienyeji.

Uchunguzi wa wa vinasaba (DNA) uliofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha bila shaka kuwa sehemu hizo za siri zilikuwa za Joyce Ludeheka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *