Kigoma. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), imekabidhi msaada wa kibinadamu kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, ili kuwasaidia wananchi waliokumbwa na mafuriko katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa zilizonyesha na yamesababisha uharibifu wa makazi na miundombinu ya msingi katika maeneo kadhaa ya manispaa hiyo.
Msaada huo unalenga kaya 283 zilizokumbwa na maafa katika kata za Katubuka, Kibirizi, Buzebazeba na Bangwe, ambazo zimeathirika zaidi. Vitu vilivyotolewa ni pamoja na mahindi tani 15.6, maharage tani 4.6, magodoro 283, blanketi 283, ndoo 283 na mikeka 283 na jumla ya waathirika ni 1,304.

Katika siku za hivi karibuni, mvua zinazoendelea kunyesha zimeendelea kuleta madhara makubwa, ikiwamo baadhi ya nyumba kujaa maji, na hivyo kulazimisha wananchi kuhama makazi yao. Pia, baadhi ya barabara na mitaro ya maji katika maeneo ya Buzebazeba, Kibirizi, Machinjioni na Bangwe zimeharibiwa na kuathiri huduma muhimu kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Andengenye ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo ya haraka ya kuwafikia waathirika. Ameeleza kuwa tayari Serikali imepeleka wataalamu kufanya utafiti wa kina katika maeneo yaliyoathirika, kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu dhidi ya mafuriko hayo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa maelekezo kwa jamii kuepuka kuendelea kuishi kwenye maeneo hatarishi, na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa ajili ya usalama wa wakazi wote wa Kigoma-Ujiji.
Mkurugenzi anayeshughulikia Operesheni na Uratibu katika Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Celestine Masalamado, amesema misaada hiyo imetolewa kufuatia ombi rasmi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, ili kuongeza nguvu katika kukabiliana na athari za mafuriko.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda ametoa pongezi kwa Serikali kwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati mgumu, akieleza kuwa kitendo hicho ni cha kiutu na kinaonesha uwajibikaji kwa wananchi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk Rashid Chuachua, ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuhakikisha misaada inawafikia walengwa, amesema atahakikisha kila kifaa kinachotolewa kinakwenda kwa wahusika waliokusudiwa.
Nelson Kubila, mkazi wa Mwanga Sokoni, amesema, “tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma. Hali ni mbaya, na tunahitaji msaada wa dhati.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, sababu kuu ya mafuriko ya kila mwaka katika eneo la Katubuka ni uwepo wa Bwawa la Katubuka, ambalo limekuwa likifurika maji. Mafuriko hayo yamesababisha hata barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa Kigoma kufungwa, na kulazimisha matumizi ya njia ya dharura.