Bahi. Ndoto nyingi za wasichana hupotea pale wanapokatisha masomo au wanapobebeshwa mimba katika umri mdogo.
Wasichana hao hulazimika kuwa kinamama katika umri mdogo huku waliowabebesha mimba wakiwakimbia.
Kwa kuliona hilo wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kuwasaidia wasichana hao ili waweze kufikia ndoto zao.
Mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya uchumi na uzazi wa mpango yaliyotolewa kwa wasichana waliopata mimba katika umri mdogo yamewawezesha kujitegemea kiuchumi kwa kuanzisha biashara baada ya kutelekezwa na waliowabebesha mimba.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 21, 2025 baadhi ya wasichana waliopata mimba katika umri mdogo wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma wamesema elimu ya ujasiriamali waliyoipata baada ya kuzalishwa na kuachwa imewasaidia.
Hawa Peter, amesema elimu ya ujasiriamali aliyoipata kutoka shirika lisilo la kiserikali la Restless Development imemsaidia kufungua biashara ya mgahawa.
Amesema alibeba ujauzito akiwa na miaka 18 na kuachwa bila msaada.

Sophia Kedmond akiwa anaendelea na shughuli za ushonaji kwenye duka lake lililopo eneo la Bahi Sokoni wilayani Bahi mkoani Dodoma.
“Sasa hivi biashara yangu ya mgahawa imekuwa kidogo kwa sababu huwa napata tenda za kulisha halmashauri kati ya watu 100 hadi 500 kwa hiyo hapa nilipo kwa sasa siyo kama nilipokuwa kabla ya kupata mafunzo, na mwanangu anasoma shule nzuri,” amesema Hawa.
Kwa upande wake Sophia Kedmond amesema alipomaliza darasa la saba alibebeshwa mimba na mwanamume aliyemkimbia.
Amesema baada ya kujifungua na kukosa cha kufanya alisikia mafunzo ya ujasiriamali yaliyokuwa yanatolewa na Shirika la Restless Development kuhusu ujasiriamali na kujitambua.
Amesema baada ya mafunzo hayo alichagua kujifunza ufundi cherehani na alihitimu na kupewa zawadi ya cherehani baada ya kufanya vizuri kwenye masomo yake.
Sophia amesema baada ya kumaliza mafunzo ya ufundi cherehani kwa miezi mitatu alikwenda kujifunza kwa vitendo na alifanya vizuri na kuwa mwanafunzi bora hivyo walimu wake walimzawadia cherehani nyingine.
Amesema baada ya kuhitimu masomo ya ufundi aliwezeshwa mtaji kidogo na mjomba wake alimpatia eneo la kujenga duka lake, na anaendelea na kazi ya kushona huku akiwa na wanafunzi wengine anaowafundisha.
“Biashara siyo mbaya sana kwa sababu huku ni kijijini biashara ya kushona nguo ni ya msimu lakini hali siyo mbaya kwa sababu naweza kuendesha maisha yangu,” amesema Sophia.
Naye Yasmin Ally amesema mafunzo ya ujasiriamali yamewasaidia kuanzisha kikundi cha kutengeneza sabuni ya maji.
Amesema kwa wiki huwa wanazalisha lita 20 na kukopesha mitaani pamoja na biashara nyingine zinazowawezesha kujikimu kimaisha.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dodoma, Amina Mafita amewataka wasichana hao kuyatumia vizuri mafunzo wanayopewa ili wajiimarishe kiuchumi.
Amewataka kufuatilia kwa ukaribu elimu ya uzazi wa mpango na kuitumia ili wasipate mimba nyingine bila kujipanga na kujipa muda mrefu kabla ya kubeba mimba nyingine.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Restless Development, Ridhiwani Juma amesema shirika hilo limefadhili mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya uchumi na elimu ya uzazi wa mpango kwa kinamama kwa mara ya kwanza ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea baada ya kupata watoto katika umri mdogo.

Hawa Peter mnufaika wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka shirika lisilo la kiserikali la Restless Development akiwa kwenye mgahawa wake Wilayani Bahi mkoani Dodoma
Amesema mafunzo hayo yamelenga wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 24.
“Mpaka sasa tuna jumla ya vijana 280 nchi nzima ambao wanapewa mafunzo ya ujasiriamali, kwa awamu hii tumewashirikisha na vijana wa kiume ili na wao wapate elimu hii ambayo itawasaidia huko mbeleni,” amesema Juma.