Waliojifungua watoto njiti waomba gharama za huduma zipungue

Arusha. Wazazi wa watoto waliolazwa katika wodi za watoto njiti wameiomba Serikali kuona namna ya kupunguza au kuondoa malipo ya gharama katika vitengo hivyo ili kuokoa maisha ya watoto wao.

Zaidi, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu zikiwemo mashine na wahudumu ili kuongeza ufanisi wa kuokoa maisha ya watoto kwa kupata huduma stahiki na kwa wakati.

Kwa wastani, gharama za matibabu katika vitengo vya watoto njiti kwa Tanzania ni Sh150, 000 hadi Sh400,000 kwa siku kutegemeana na tatizo alilonalo mtoto aliyezaliwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Kimataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), watoto zaidi ya 250,000 huzaliwa wakiwa njiti kila mwaka nchini Tanzania na takribani 9,500 kati yao hupoteza maisha.

Wazazi hao wametoa ombi hilo kwa Serikali leo Machi 12, 2025, jijini Arusha, wakati wakipokea msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kupunguza gharama za kuishi hospitalini ulitolewa na wanawake wa kikundi cha Arusha Super Women katika Hospitali ya Mount Meru.

Stellah John, mmoja wa wazazi hao, amesema kuwa watoto njiti wanahitaji huduma maalumu na matibabu ya haraka, lakini gharama za huduma hizo ni kubwa.

“Gharama kubwa imekuwa changamoto kwa wazazi, huku wengi wao wakikosa uwezo wa kifedha kumudu huduma za afya zinazohitajika haraka kwa watoto, hivyo tunaomba Serikali ione umuhimu wa kupunguza au kuondoa kabisa gharama hizi ambazo zinasababisha hata msongo wa mawazo kwa mama aliyejifungua na magonjwa kama shinikizo la juu la damu.”

Mzazi mwingine, Rebecca Eliezer, ameongeza kuwa Serikali inahitaji kuongeza nguvu katika kitengo cha watoto njiti, hasa katika kuboresha miundombinu na kuongeza wahudumu na mashine zinazohitajika kwa ajili ya matibabu.

“Pamoja na huduma kuwa ghali, bado wahudumu na mashine ni chache na haikidhi mahitaji ya watoto kutokana na idadi kubwa tuliyoko hapa,” amesema.

“Serikali inapaswa kuhakikisha pia kitengo na huduma hii inapatikana katika hospitali za wilaya ili kupunguza mlundikano katika hospitali kubwa kama ya Mount Meru,” amesema Rebecca.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Charles Mkombachepa, pamoja na kusema kwamba hospitali zote za wilaya zina vitengo vya watoto njiti, bado kuna upungufu wa vifaa muhimu.

“Hakuna hospitali ya wilaya isiyo na kitengo cha watoto njiti, lakini changamoto kubwa ni upungufu wa vifaa na miundombinu, hii ndiyo sababu baadhi ya watoto hulazimika kupatiwa rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya Mount Meru,” amesema Dk Mkombachepa.

Amesema Serikali inaendelea kushughulikia suala hilo ili kuhakikisha huduma ya watoto wanaozaliwa na wanaotarajia kuzaliwa inakuwa salama.

Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Arusha Super Women,’ Bertha Kondo, amesema wameamua kutoa msaada huu kwa wazazi na wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kama sehemu ya kutekeleza mpango wao wa kugusa maisha ya jamii.

“Tumekuwa tukitoa misaada katika kambi mbalimbali na magereza, lakini awamu hii tumekuja hapa Mount Meru ili kuwatembelea wagonjwa, kuwafariji katika kipindi kigumu wanachopitia, na pia kutoa msaada wa vitu mbalimbali vya usafi, lishe na kujisitiri,” amesema Bertha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *