Walioingilia mfumo ya benki, kujipatia Sh2 bilioni wakosa dhamana

Dar es Salaam. Raia wa Ghana, Valentine Kofi (45) na Watanzania watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2 bilioni, mali ya benki ya Banc ABC.

 Mbali na Kofi ambaye ni mkazi ya Mikocheni washtakiwa wengine ni Patrick Tarimo (34) mkazi wa Kibaha, Aisha Kagashe (40) mkazi wa Sinza na Idan Msuya (46) mkazi wa Mikocheni.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Machi 13, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru amewasomea mashitaka yao, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Kabla ya kusomewa mashitaka yao, Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa hao kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Pia, shitaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika shitaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Septemba Mosi, 2021 na Oktoba 25, 2021 ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi tisa za Afrika ambazo ni Ghana, Ivory Coast, Uganda, Zambia, Senegal, Cameroon, Ufaransa, Mali na Bukinafaso.

Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliongoza genge hilo kwa kuingilia mfumo wa benki ya African Banking Corporation of Tanzania Limited( Banc ABC), kwa lengo la kuiba Sh2.09 bilioni mali ya benki hiyo.

Shitaka la pili ni kuingilia mfumo wa benki, ambapo washtakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani siku na maeneo halo, waliingilia mfumo wa kompyuta wa benki hiyo na kudukua akaunti 160 za visa za malipo ya awali zilizopo katika benki hiyo na kusababisha benki hiyo ipate deni la Sh3.54 bilioni.

Shitaka la tatu ni wizi, tukio wanalodaiwa kulitenda Oktoba 24 na Oktoba 25, 2021 katika maeneo hayo, ambapo washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliiba Sh2.09 bilioni kupitia kadi ya visa ya malipo ya awali kutoka katika benki hiyo.

Shitaka la nne ni kutakatisha fedha, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 24, 2021 na Februari 18, 2025 katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi hizo, washtakiwa kwa pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, walijipatia Sh2 bilioni mali ya benki ya Banc ABC, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la wizi.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *