Morogoro. Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali iliyohusisha malori mawili yaliyogongana na kuwaka moto mkoani hapa, imeongezeka na kufikia watu watatu.
Miili hiyo bado haijatambuliwa kutokana na kuteketea kabisa, hivyo uchunguzi wa kitaalamu unaendelea ili ndugu waitambue.
Akizungumzia ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo Machi 4, 2025, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo Amesema awali wakiwa eneo la ajali, walifanikiwa kupata miili miwili.

Malori mawili yakiteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso eneo la nane nane barabara ya Morogoro -Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo na kusababisha Vifo vya watu watatu. Picha Jackson John, Mwananchi
Hata hivyo, baada ya kumaliza kuzima moto katika malori hayo, amesema walifanikiwa kupata mwili mwingine mmoja na hivyo kufanya jumla ya miili mitatu iliyopatikana kwenye ajali hiyo.
“Miili hiyo yote bado haijatambulika kwa majina wala jinsia kutokana na kuteketea kabisa kwa moto, hata hivyo uchunguzi wa kitaalamu unaendelea ili kuitambua na kwa sasa imepelekwa kuhifadhia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro,” amesema Kamanda Marugujo.
Marugujo ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pindi yanapotokea majanga kama hayo, ili kuwezesha hatua za haraka za uokoaji.

Wananchi wakishuhudia moto ukiteketeza malori mawili yaliyogongana uso kwa uso na kuwapa moto eneo la nane nane barabara ya Morogoro – Dar es Salaam. Picha Jackson John, Mwananchi
“Taarifa zilichelewa kutufikia, hata hivyo baada ya kupata taarifa za ajali hiyo mara moja tulifika eneo la tukio, lakini tayari tulikuta moto mkubwa na ulikuwa ukisambaa kwa kasi, tulipambana mpaka tumefanikiwa kuuzima,” amesema Marugujo.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Linus Mnyambwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori la mizigo lililokuwa likitokea Msamvu, ambaye hakuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kutaka kulipita gari la mbele yake bila kuchukua tahadhari, hivyo kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.

Malori mawili yakiteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso eneo la nane nane barabara ya Morogoro -Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo na kusababisha Vifo vya watu watatu. Picha Jackson John, Mwananchi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuzuia ajali zinazotokana na uzembe.