Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa matokeo ya usaili wa maandishi uliofanyika Machi 29 na 30, 2025 kwa watahiniwa walioomba nafasi za kazi TRA yatatangazwa Aprili 25 baada ya kuwasilishwa na mshauri elekezi Aprili 23, 2025.
Akizungumzia mchakato huo leo Jumatano Aprili 2, 2025 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala, Moshi Kabengwe amesema baada ya majina kutangazwa usaili wa vitendo na mahojiano utafuata.
Kabengwe amesema usaili wa vitendo utaanza Mei 2, 2025 hadi 4 kwa kada ya madereva na waandishi waendesha ofisi, huku usaili wa mahojiano kwa kada nyingine utafanyika kuanzia Mei 7 hadi 9.
Pia, ameeleza kuwa watakaofanikiwa kupita katika hatua hiyo wataarifiwa Mei 18, 2025 na kuanza mafunzo elekezi Mei 22 hadi Juni 2, 2025 watakapoajiriwa na kuanza kazi rasmi.
“Katika mchakato wa usaili maombi yaliyokidhi vigezo yalikuwa 112,952 yakaongezeka maombi 71 baada ya kukata rufaa na kufikisha idadi ya maombi 113,023 yaliyohusisha waombaji 86,314 na waliofanya usaili wa maandishi ni waombaji 78,544 sawa na asilimia 91 ya waombaji wote.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala, Moshi Kabengwe
“Waombaji 7,770 sawa na asilimia 9 hawakufika kwenye usaili kwa sababu mbalimbali. Sera ya TRA ni ajira sawa kwa wote na zilizotangazwa zitazingatia sifa na vigezo vya muomba kazi bila kujali hali ya muhusika kwamba ni mtoto wa maskini, wa kiongozi au wa mtumishi wa umma, ndiyo maana vituo vya usaili viliwekwa kwenye mikoa minane na Zanzibar ili kusogeza huduma karibu,”amesema na kuongeza Kabengwe