‘Walimu wasiosimamia adhabu ya viboko waondolewe’

Simiyu. Serikali imeshauriwa kuwaondoa katika nafasi zao walimu wakuu na wakuu wa shule za msingi na sekondari ambao watashindwa kusimamia utoaji wa adhabu ya viboko kwa wanafunzi kwa kufuata Waraka wa Elimu Namba 24.

Ushauri huo umetolewa baada ya ongezeko la matukio ya udhalilishaji na madhara kwa wanafunzi yanayosababishwa na adhabu hizo, hasa baada ya tukio la mwanafunzi wa shule ya Sekondari Mwasamba, Busega Mkoa wa Simiyu, Mhoja Maduhu (18) kuuawa kwa fimbo hivi kabuni.

Ushauri huu umetolewa huku kukiwa na waraka huo ambao unaelekeza utaratibu wa utoaji wa adhabu hiyo.

Waraka huu unatoa maelekezo kwamba adhabu hiyo inapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu kwa maandishi.

Aidha, mwanafunzi wa kike anapaswa kupigwa viboko na mwalimu wa kike isipokuwa pale ambapo shule haina mwalimu wa kike.

Pia, waraka unasisitiza kwamba kila adhabu ya viboko itarekodiwa kwa kina katika kitabu maalumu, ikijumuisha jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu hiyo, mambo ambayo hayazingatiwi.

Kufuatia hali hiyo, wadau wa elimu katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wamelieleza Mwananchi leo Jumapili Machi 9, 2025 kuwa Serikali inatakiwa iwavue uongozi walimu wanaokiuka utaratibu wa adhabu ya viboko.

Wadau wa elimu katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, wamesema kuwa utoaji wa adhabu ya viboko umegeuka kuwa mateso kwa wanafunzi, huku baadhi yao wakipata madhara kama vile kuvunjika mikono, majeraha ya mwili na hata kifo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Maswa, Basila Bruno amesisitiza kuwa hata sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inakataza ukatili wa aina yoyote kwa mtoto.

Amesema sheria hiyo inasema kwamba adhabu ya viboko inayoruhusiwa ni ile ya viboko vinne tu kwa wavulana (makalioni) na mikononi kwa wasichana, na kila adhabu inapaswa kurekodiwa kwa usahihi.

“Lakini, kutokana na kutofuata sheria hii, baadhi ya walimu wanakiuka taratibu na kufanya vitendo vya kikatili,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe amesisitiza kuwa adhabu ya viboko bado ina umuhimu na inatakiwa kutolewa kwa wanafunzi waliokosa nidhamu.

Hata hivyo, amesema kuwa walimu wanapaswa kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa kutoa adhabu hii kwa umakini ili kuepuka madhara.

Mkazi wa Maswa, Slivester Lugembe, amesema kuwa utaratibu wa adhabu ya viboko unakiukwa na wanafunzi wanapigwa hovyo, huku wengine wakipigwa ngumi na mateke, jambo ambalo linahatarisha uhusiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.

Mkazi mwingine wa Wilaya ya Maswa, Mary Samson, amesema kuwa idadi kubwa ya walimu wamegeuza adhabu ya viboko kuwa vipigo vya ngumi na mateke, jambo linalochangia kuvuruga nidhamu.