Walimu mbaroni wakidaiwa kutumia tamthilia, mpira kubaka wanafunzi

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu wakiwemo walimu wawili kwa tuhuma za kubaka wanafunzi kwa nyakati tofauti.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa kupitia taarifa aliyoitoa Machi 19, 2025, amedai tukio la kwanza lilitokea Februari 24, mwaka huu saa tano asubuhi ambapo mwanafunzi wa kidato cha tatu (16) anadaiwa kubakwa na mwalimu wa Shule ya Msingi Nyampande wakati akiangalia mpira nyumbani kwa mwalimu huyo, katika kijiji cha Nyampande wilayani Sengerema.

“Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na desturi ya kwenda kutazama televisheni nyumbani kwa mwalimu Edwin Temba, ambapo Februari 24, 2025, saa tano asubuhi mwanafunzi huyo alikwenda kwa mwalimu Temba kutazama mpira wa miguu, ndipo mtuhumiwa huyo alipopata nafasi ya kumbaka na kumfanyia kitendo hicho cha kikatili,” Mutafungwa.

Amedai mtuhumiwa huyo amekamatwa na upelelezi utakapo kamilika atafikishwa mahakamani.

Katika tukio la pili, Mutafungwa amesema jeshi hilo pia linamshikilia mwalimu wa Shule ya Msingi Bukala, Daudi Ochieng (37) na Adon Sospeter (53) wakazi wa Ibisabageni Wilaya ya Segerema  kwa tuhuma za kumbaka kwa  nyakati tofauti mwanafunzi wa umri wa miaka 10.

“Oktoba, 2024 hadi Februari, 2025 mmiliki wa nyumba anamoishi mwathirika wa tukio hilo, Adon Sospeter kwa nyakati tofauti alimfanyia kitendo cha kikatili kwa kumbaka mtoto huyo ambapo alimuita ndani ya chumba chake wakaangalie tamthilia kwa pamoja. Alidai mtu huyo aliendelea kumfanyia kitendo hicho mara kwa mara hadi ilipobainika Februari, 2025,”amesema Mutafungwa.

Ameeleza, mtoto huyo pia alifanyiwa ukatili huo na mwalimu wake Februari, mwaka huu baada ya kumuita  nyumbani kwake amfundishe masomo ya ziada, badala yake inadaiwa aliingiwa tamaa na kumbaka.

Mutafungwa amesema Februari 26, 2025 mama mzazi wa mtoto huyo aligundua afya ya mtoto wake imedhoofika ndipo alipoamua kumpeleka hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu.

“Baada ya uchunguzi kwa mtoto huyo, ilibainika kuwa na michubuko sehemu zake za siri ndipo mzazi wake aliamua kutoa taarifa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sengerema ambapo uchunguzi ulianza kwa kuwatafuta watuhumiwa wa tukio hilo,”amedai Mutafungwa.

Ameongeza kuwa, siku hiyohiyo jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote wawili waliofanya kitendo hicho na wapo mahabusu ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Sengerema,  watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika. 

Matukio hayo ni mwendelezo wa vitendo vya ukatili kwa watoto, ambapo hivi karibuni jeshi hilo lilisema zaidi ya watoto 641 wamefanyiwa ukatili ndani ya miezi tisa, kuanzia Oktoba 2023 hadi Juni, 2024 katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela jijini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *